Maajabu ya Uumbaji Humtukuza Yehova
Maajabu ya Uumbaji Humtukuza Yehova
YEHOVA MUNGU ni mkuu zaidi kuliko vile wanadamu wasio wakamilifu wanavyoweza kuwazia. Uumbaji wake hapa duniani na mbinguni humletea sifa na kutufanya tumheshimu.—Zaburi 19:1-4.
Akiwa Muumba na Mwenye Enzi Kuu ya Ulimwengu Wote, bila shaka, Yehova anastahili kusikilizwa anapozungumza. Hata hivyo, tunazweza kustaajabu sana Mungu akizungumza nasi wanadamu duni hapa duniani! Tuseme kwamba Mungu angezungumza nawe, labda kupitia malaika. Bila shaka, ungesikiliza. Haikosi kwamba yule mwanamume mnyoofu Ayubu alisikiliza kwa makini sana Mungu alipozungumza naye miaka 3,500 hivi iliyopita. Tunaweza kujifunza nini kutokana na maneno ambayo Mungu alimwambia Ayubu kuhusu dunia na mbingu zinazoonekana?
Ni Nani Aliyeiumba Dunia, na Ni Nani Anayeiongoza Bahari?
Kutoka katika dhoruba ya upepo, Mungu anamuuliza Ayubu kuhusu dunia na bahari. (Ayubu 38:1-11) Hakuna mwanadamu yeyote ambaye ni mtaalamu wa kuchora ramani za ujenzi aliyeamua dunia inapaswa kuwa na ukubwa gani kisha akasaidia kuiumba. Akilinganisha dunia na jengo, Mungu anamuuliza Ayubu hivi: “Ni nani aliyeweka jiwe lake la pembeni?” Si mwanadamu! Malaika ambao ni wana wa Mungu walitazama na kushangilia Yehova alipoiumba dunia.
Bahari ni kama kitoto kichanga ikilinganishwa na Mungu ambaye huivika vazi kwa njia ya mfano. Ilianza “kwenda kama katika wakati ilipotoka katika tumbo la uzazi.” Mungu huizuia bahari kana kwamba kwa pingo na milango iliyofungwa, nayo mawimbi yanaongozwa kwa nguvu za mwezi na jua.
Kitabu kimoja (The World Book Encyclopedia) kinasema hivi: “Upepo husababisha mawimbi mengi ya bahari, kuanzia mawimbi madogo sana hadi mawimbi makubwa ya kimbunga yaliyo na kimo cha zaidi ya meta 30. . . . Baada ya upepo kutulia, mawimbi huendelea kusonga juu ya uso wa bahari na yanaweza kusafiri mbali sana kutoka yalipoanzia. Mawimbi hayo huwa matulivu na marefu zaidi. Hatimaye, mawimbi hufika ufuoni ambako huvunjika na kufanyiza povu.” Bahari inatii amri hii ya Mungu: “Unaweza kufika hapa, na usipite; na hapa mawimbi yako yenye fahari yamewekewa mpaka.”
Ni Nani Anayeleta Mapambazuko?
Kisha Mungu anamuuliza Ayubu kuhusu kazi za nuru na kuhusu vitu vingine ambavyo ameumba. (Ayubu 38:12-18) Hakuna mwanadamu anayeweza kutokeza usiku na mchana. Kwa njia ya mfano, nuru ya asubuhi hushika miisho ya dunia na kuikung’uta ili kuwaondoa waovu. Huenda watenda-dhambi wakafanya matendo ya ukosefu wa uadilifu katika “giza la jioni.” (Ayubu 24:15, 16) Lakini watenda-maovu wengi hutawanyika kunapopambazuka.
Nuru ya asubuhi ni kama muhuri mkononi mwa Mungu ambao unaifanya dunia ivutie kana kwamba imepigwa muhuri na Mungu. Jua hutokeza rangi nyingi hivi kwamba dunia huonekana kuwa imepambwa kwa vazi maridadi. Ayubu hakuhusika katika uumbaji huo wala hakuwa ametembea katika vilindi vya maji ili kuorodhesha hazina zake. Naam, kufikia leo, watafiti hawajui mambo yote kuhusu viumbe wa baharini!
Ni Nani Aliye na Maghala ya Theluji na ya Mvua ya Mawe?
Hakuna mtu ambaye amewahi kuisindikiza nuru au giza mpaka nyumbani kwake wala hakuna yule aliyewahi kuingia kwenye maghala ya theluji na ya mvua ya mawe ambayo Mungu ameyaweka kwa ajili ya “siku ya pigano na vita.” (Ayubu 38:19-23) Yehova alipotumia mvua ya mawe dhidi ya adui zake huko Gibeoni, “wale waliokufa kutokana na hayo mawe ya mvua walikuwa wengi kuliko wale ambao wana wa Israeli waliwaua kwa upanga.” (Yoshua 10:11) Huenda akatumia mawe ya mvua yaliyo na ukubwa usiojulikana ili kuwaharibu wanadamu waovu wanaoongozwa na Gogu, yaani, Shetani.—Ezekieli 38:18, 22.
Mnamo Julai 2002, mawe ya mvua yenye ukubwa wa yai la kuku yaliwaua watu 25 na kuwaumiza wengine 200 katikati ya Mkoa wa Henan huko China. Mchongaji wa sanamu Mwitaliano, Benvenuto Cellini, aliandika hivi kuhusu dhoruba ya mvua ya mawe iliyotukia mwaka wa 1545: “Tulikuwa mbali sana na mji wa Lyons . . . wakati mbingu zilipoanza kunguruma kwa sauti kubwa. . . . Baada ya ngurumo kukawa na sauti kubwa yenye kushtua sana, nikafikiri siku ya mwisho imefika; basi nikasimamisha kidogo farasi wangu, huku mvua ya mawe ikinyesha bila tone la maji kuanguka. . . . Kisha mawe hayo yakawa makubwa kama malimau. . . . Hiyo dhoruba iliendelea kwa muda, lakini mwishowe ikakwisha . . . Tulionyeshana mikwaruzo na majeraha yetu; lakini tuliposonga mbele kidogo tuliona uharibifu mkubwa sana kuliko ule uliotupata, ambao hauwezi kuelezeka. Miti yote ilikuwa imeanguka pamoja na majani yake yote; wanyama waliokuwa shambani walikufa; wachungaji wengi pia walikufa; tuliona mawe mengi makubwa ya mvua ambayo hayangeweza kubebwa kwa mikono miwili.”—Autobiography (Kitabu cha 2, 50), Harvard Classics, Buku la 31, ukurasa wa 352-353.
Itakuwaje Yehova atakapofungua maghala yake ya theluji na ya mawe ya mvua juu ya adui zake? Bila shaka, hawataokoka wakati theluji au mawe ya mvua yatakapotumiwa kutimiza mapenzi yake.
Ni Nani Aliyefanyiza Mvua, Umande, Sakitu, na Barafu?
Kisha Yehova anamuuliza Ayubu kuhusu mvua, umande, sakitu, na barafu. (Ayubu 38:24-30) Mungu ndiye hutengeneza mvua, na hata “nyika isiyokuwa na mtu wa udongo” hufurahia baraka zake. Mvua, barafu, na sakitu havina baba wa kibinadamu au mwanzilishi wa kibinadamu.
Jarida fulani (Nature Bulletin) linasema hivi: “Jambo la kushangaza zaidi au labda muhimu zaidi [kuhusu barafu] ni kwamba maji hupanuka yanapoganda . . . Tabaka la barafu ambalo hufanyizwa na kuelea katika bwawa wakati wa baridi kali huwezesha mimea na viumbe (samaki, n.k.) walio ndani ya maji kuendelea kuishi chini ya maji. Ikiwa . . . maji yangekuwa mazito yanapoganda na ikiwa hayangepanuka, barafu ingekuwa nzito kuliko maji na ingezama. Barafu ingezidi kufanyizwa juu ya maji hivi kwamba bwawa lingeganda kabisa. . . . Katika sehemu za dunia zenye baridi, barafu ingejaa daima katika mito, mabwawa, maziwa, na hata bahari.”
Tunapaswa kushukuru kwamba sehemu zenye maji duniani huwa hazigeuki kuwa barafu kabisa! Na bila shaka, tunashukuru kwamba mvua na umande, ambazo Yehova alifanya, huikuza mimea ya dunia.
Ni Nani Aliyetunga Sheria za Mbingu?
Kisha Mungu anamuuliza Ayubu kuhusu mbingu. (Ayubu 38:31-33) Kwa kawaida, kundi-nyota la Kima siku hizi hutambulishwa kuwa Pleiades, ambacho ni kikundi chenye nyota saba kubwa na nyingine ndogo zilizo umbali wa miaka ya nuru 380 hivi kutoka kwenye jua. Mwanadamu hawezi “kufunga vifungo vya kundi-nyota la Kima,” yaani, kufunga nyota hizo pamoja. Hakuna mwanadamu anayeweza “kufungua kamba za kundi-nyota la Kesili,” ambalo siku hizi hutambulishwa kuwa Orion. Ingawa kwa sasa makundi-nyota ya Mazarothi na Ashi hayajatambuliwa, mwanadamu hawezi kuyadhibiti na kuyaongoza. Wanadamu hawawezi kubadili “sheria za mbingu” ambazo zinaongoza ulimwengu.
Mungu alitunga sheria ambazo zinaongoza vitu vya angani, ambavyo hubadili halihewa ya dunia, mawimbi, angahewa, na hata uhai duniani. Fikiria jua. Kitabu kimoja (The Encyclopedia Americana, chapa ya 1996) kinasema hivi kuhusu jua: “Miale ya jua huiwezesha dunia kupata joto na nuru, husaidia mimea kukua, hufanya maji yaliyo katika bahari na katika sehemu nyingine yawe mvuke, huhusika katika kutokeza
upepo, na hufanya mambo mengine mengi ambayo ni muhimu ili kuendeleza uhai duniani.” Kitabu hichohicho kinasema hivi: “Ili kuelewa nguvu nyingi zilizo katika mwangaza wa jua, inafaa kukumbuka kwamba nguvu zote zilizo katika upepo, mabwawa, na mito na nguvu zilizo katika vyanzo vya asili vya nishati kama vile mbao, makaa, na mafuta zinatokana na mwangaza wa jua ambao umehifadhiwa na sayari ndogo [dunia] iliyo umbali wa kilometa milioni 150 kutoka kwenye jua.”Ni Nani Aliyetia Hekima Katika Mawingu?
Yehova anamwambia Ayubu afikirie mawingu. (Ayubu 38:34-38) Mwanadamu hawezi kuamuru hata wingu moja litokee na kutoa maji yake. Lakini wanadamu wanategemea sana mzunguko wa maji ambao Muumba ameumba!
Mzunguko wa maji ni nini? Kitabu kimoja kinasema hivi: “Mzunguko wa maji hutimiza mambo manne muhimu: kuhifadhi, kufanyiza mvuke, kunyesha, na kutengeneza mito. Maji yanaweza kuhifadhiwa udongoni kwa muda; kwenye bahari, maziwa, na mito; na kwenye vilele vya barafu na mito ya barafu. Yakiwa mvuke yanatoka kwenye uso wa dunia, yanaganda mawinguni, yanarudi duniani yakiwa mvua au theluji, na hatimaye yanaenda baharini au yanakuwa mvuke tena na kurudi kwenye angahewa. Karibu maji yote duniani yamepitia mzunguko huo wa maji mara nyingi sana.”—Microsoft Encarta Reference Library 2005.
Mawingu yenye mvua ni kama mitungi ya maji ya mbinguni. Yehova anapoipindua, inaweza kumwaga mvua nyingi sana na kuigeuza vumbi kuwa matope. Mungu anaweza kutokeza mvua au kuizuia.—Yakobo 5:17, 18.
Mara nyingi mvua huambatana na umeme, hata hivyo mwanadamu hawezi kuutumia kutimiza makusudi yake. Umeme unatajwa ukimwambia Mungu hivi: “Sisi tupo hapa!” Kitabu kimoja (Compton’s Encyclopedia) kinasema hivi: “Umeme husababisha mabadiliko makubwa ya kikemikali katika angahewa. Umeme unapopita hewani, hutokeza joto jingi sana ambalo huunganisha nitrojeni na oksijeni ili kufanyiza naitreti na kemikali nyingine. Michanganyiko hiyo huanguka Duniani pamoja na mvua. Hivyo, angahewa huendelea kutokeza vitu ambavyo udongo unahitaji ili kuzalisha mimea.” Mwanadamu hajui mambo yote kuhusu umeme, lakini Mungu anayajua.
Maajabu ya Uumbaji Yanamletea Mungu Sifa
Naam, maajabu ya uumbaji humtukuza Muumba wa vitu vyote. (Ufunuo 4:11) Haikosi Ayubu alivutiwa sana na maneno ya Yehova kuhusu dunia na vitu vingine vilivyo angani!
Tumezungumzia tu baadhi ya maajabu ya uumbaji ambayo Ayubu alielezwa katika maswali aliyoulizwa. Lakini, hata yale ambayo tumezungumzia yanatuchochea kusema hivi: “Tazama! Mungu ameinuliwa sana kuliko tunavyoweza kujua.”—Ayubu 36:26.
[Picha katika ukurasa wa 14]
Snowflake: snowcrystals.net
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Pleiades: NASA, ESA and AURA/Caltech; fish: U.S. Fish & Wildlife Service, Washington, D.C./William W. Hartley