Nimeona Kundi la Mungu Likikua Nchini Korea
Nimeona Kundi la Mungu Likikua Nchini Korea
Limesemuliwa na Milton Hamilton
“Tunasikitika kuwajulisha kwamba serikali ya Jamhuri ya Korea imefutilia mbali viza zenu ninyi nyote wamishonari na imeamua kwamba hamruhusiwi kuingia Korea. . . . Kutokana na mabadiliko hayo, mmepata mgawo wa kutumika nchini Japani kwa muda.”
MWISHONI mwa mwaka wa 1954, mimi na mke wangu tulipokea ujumbe ulio hapo juu kutoka Brooklyn, New York, Marekani. Mwanzoni mwa mwaka huo, tulihitimu katika darasa la 23 la Shule ya Gileadi kaskazini mwa New York. Tulipopokea barua hiyo, tulikuwa tukitumikia kwa muda huko Indianapolis, Indiana.
Mimi na mke wangu, Liz (zamani aliitwa Liz Semock), tulisomea katika darasa moja la sekondari. Baadaye, tulifunga ndoa mwaka wa 1948. Alipenda huduma ya wakati wote lakini aliogopa kutoka Marekani na kuhamia nchi ya kigeni. Kwa nini alibadili maoni yake?
Liz alikubali kuambatana nami katika mkutano wa wale waliotaka kuwa wanafunzi wa Gileadi. Mkutano huo ulifanywa wakati wa kusanyiko la kimataifa katika Uwanja wa Yankee, New York, katika majira ya kiangazi ya mwaka wa 1953. Baada ya kuhudhuria mkutano huo wenye kutia moyo, tulijaza maombi ya Gileadi. Jambo la kushangaza ni kwamba tulialikwa kuhudhuria darasa linalofuata, kuanzia Februari 1954.
Tulitumwa Korea, vita vya miaka mitatu ambavyo viliharibu kabisa nchi ya Korea vilikuwa tu vimekwisha katika majira ya kiangazi ya 1953. Tulifuata maagizo ya barua tuliyopokea na kwenda kwanza nchini Japani. Baada ya kusafiri kwa meli kwa siku 20, tulifika Japani mnamo Januari 1955 pamoja na wamishonari wenzetu sita ambao pia walikuwa wametumwa Korea. Lloyd Barry, aliyekuwa mwangalizi wa ofisi ya tawi ya Japani wakati huo, alikutana nasi bandarini saa 12 asubuhi. Tulifunga safari ya kwenda kwenye makao ya wamishonari huko Yokohama. Baadaye siku hiyo, tulienda kuhubiri.
Mwishowe Tunaingia Korea
Baada ya muda, tulipata viza za kuingia katika Jamhuri ya Korea. Mnamo Machi 7, 1955, ndege tuliyopanda iliondoka katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Haneda huko Tokyo na kupaa kwa saa tatu mpaka Uwanja wa Ndege wa Yoido huko Seoul. Mashahidi zaidi ya 200 wa Korea walitukaribisha, na tulitokwa na machozi ya shangwe. Kulikuwa na Mashahidi 1,000 tu katika nchi yote ya Korea wakati huo. Kama watu wengine wengi wa nchi za Magharibi, tulifikiri kwamba watu wote wa nchi za Mashariki wanafanana na wanatenda kwa njia ileile hata iwe
wametoka nchi gani. Punde si punde, tuligundua kwamba hawafanani. Wakorea wana lugha yao, alfabeti yao, vyakula vyao, sura yao ni tofauti, wana mavazi yao ya kitamaduni, na vitu vingine ambavyo ni vya Korea tu, kama vile mtindo wao wa ujenzi.Kwanza, tulikuwa na kazi ngumu ya kujifunza Kikorea. Hatukuwa na vitabu vya kujifunzia Kikorea. Muda si muda, tuligundua kwamba hatuwezi kutamka maneno ya Kikorea tukitumia matamshi ya Kiingereza. Mtu anaweza kujifunza matamshi yanayofaa kwa kujifunza tu alfabeti ya Kikorea.
Tulikosea-kosea. Kwa mfano, Liz alimuuliza mwenye nyumba fulani ikiwa ana Biblia. Mtu huyo alimtazama kwa mshangao, akaondoka na kurudi akiwa na kibweta cha viberiti. Kumbe Liz alikuwa amemwomba alete sungnyang (viberiti) badala ya sungkyung, neno linalomaanisha “Biblia.”
Baada ya miezi michache, tulipewa mgawo wa kufungua makao ya wamishonari huko Pusan, jiji lenye bandari lililo upande wa kusini. Tulikodi vyumba vitatu vidogo kwa ajili yetu wawili na dada wengine wawili waliotumwa huko pamoja nasi. Vyumba hivyo havikuwa na maji ya bomba wala choo cha maji. Maji yaliweza tu kupanda juu kwenye ghorofa ya pili wakati wa usiku yalipoongezeka. Kwa hiyo, tulikuwa tukiamka kwa zamu usiku wa manane ili kujaza mitungi maji. Tulilazimika kuchemsha maji au kuyasafisha kwa klorini ili yawe safi.
Kulikuwa na matatizo mengine. Hatungeweza kutumia mashini ya kufulia nguo wala kupiga pasi kwa sababu umeme haukutosha. Tulipikia kwenye veranda, na kifaa pekee tulichotumia ni jiko la mafuta. Punde si punde, kila mmoja wetu alijifunza kupika chakula kwa jiko hilo wakati wa zamu yake. Baada ya miaka mitatu, mimi na Liz tulipata ugonjwa wa ini. Katika miaka hiyo, wamishonari wengi walipatwa na ugonjwa huo. Tulipona baada ya miezi mingi, na tulipata matatizo mengine ya kiafya.
Wasaidiwa Kushinda Vipingamizi
Katika miaka 55 ambayo imepita, rasi ya Korea imekumbwa na misukosuko mingi ya kisiasa huko Asia. Eneo lisilo na majeshi limegawanya rasi hiyo katikati. Eneo hilo liko kilomita 55 upande wa kaskazini wa Seoul, mji mkuu wa Jamhuri ya Korea. Mwaka wa 1971, Frederick Franz kutoka katika makao makuu ya Brooklyn alitembelea nchi hiyo. Niliambatana naye katika eneo lisilo na majeshi. Eneo hilo limelindwa kutokana na mashambulizi kuliko eneo lingine lolote duniani. Kwa miaka mingi, maofisa wa Umoja wa Mataifa wamekutana huko mara nyingi na wawakilishi wa serikali zote mbili.
Bila shaka, hatuungi mkono upande wowote wa kisiasa katika ulimwengu huu, kutia ndani na Yoh. 17:14) Kwa sababu ya kukataa kuchukua silaha na kuwashambulia wanadamu wenzao, Mashahidi wa Korea zaidi ya 13,000 wamefungwa gerezani kwa jumla ya miaka 26,000. (2 Kor. 10:3, 4) Ndugu wote vijana katika nchi hiyo wanajua kwamba watakabili suala hilo, lakini hawaogopi. Inahuzunisha kwamba serikali inawaita wahudumu Wakristo “wahalifu” lakini “uhalifu” pekee ambao inadai wametenda ni kukataa kulegeza msimamo wao wa Kikristo wa kutounga mkono upande wowote katika vita.
siasa za rasi ya Korea. (Katika mwaka wa 1944, wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, mimi pia nilikataa kutumikia katika jeshi na hivyo nikafungwa kwa miaka miwili na nusu katika gereza la Lewisburg, Pennsylvania, huko Marekani. Kwa hivyo, ingawa ndugu zetu wa Korea wameteseka zaidi gerezani, ninaelewa mateso ambayo Mashahidi hao vijana wamekabili. Nilitiwa moyo sana kujua kwamba wamishonari wengine kati yetu nchini Korea walikabili hali kama hiyo.—Isa. 2:4.
Tunakabili Hali Ngumu
Msimamo wetu wenyewe wa kutounga mkono upande wowote ulijaribiwa na suala fulani mwaka wa 1977. Maofisa waliwazia kwamba tulikuwa tumewachochea vijana Wakorea wakatae kujiunga na jeshi na kuchukua silaha. Kwa hivyo, serikali iliamua kuwanyima viza za kurudi nchini wamishonari waliotoka nchini kwa sababu yoyote ile. Amri hiyo ilidumu kuanzia 1977 mpaka 1987. Ikiwa tungeondoka Korea miaka hiyo, hatungeruhusiwa kurudi. Kwa hiyo, katika miaka hiyo hatukwenda nyumbani hata kwa ajili ya matembezi tu.
Tulikutana mara nyingi na maofisa wa serikali na kuwaeleza kwamba tukiwa wafuasi wa Kristo hatuungi mkono upande wowote katika siasa. Mwishowe, waligundua kwamba hatukuogopa, kwa hivyo, waliondoa amri hiyo, baada ya miaka kumi. Katika miaka hiyo, wamishonari wachache walilazimika kuondoka nchini kwa sababu mbalimbali kama vile ugonjwa, lakini wengine wetu tulibaki, na tunafurahi kwamba tulifanya hivyo.
Katikati ya miaka ya 1980, watu waliopinga huduma yetu waliwashtaki kwa uwongo wakurugenzi wa shirika letu la kisheria kwamba wanawafundisha vijana kukataa kujiunga na jeshi. Mara moja, serikali ilimwita kila mmoja wetu na kumhoji. Mnamo Januari 22, 1987, ofisi ya kuendesha mashtaka ilipata kwamba mashtaka hayo hayakuwa na msingi. Hilo lilisaidia kusahihisha maoni yoyote yasiyofaa yaliyotokea baadaye.
Mungu Anabariki Kazi Yetu
Kadiri miaka ilivyopita, kazi yetu ya kuhubiri ilizidi kupingwa huko Korea kwa sababu ya msimamo wetu wa kutounga mkono upande wowote. Hivyo, ilikuwa vigumu zaidi kupata mahali panapofaa pa kufanyia makusanyiko yetu makubwa. Kwa hiyo, Mashahidi walisuluhisha tatizo hilo kwa kujenga Jumba la Kusanyiko huko Pusan. Lilikuwa jumba la kwanza kabisa katika nchi za Mashariki. Nilikuwa na pendeleo la kutoa hotuba ya wakfu Aprili 5, 1976 (5/4/1976), mbele ya wasikilizaji 1,300.
Kuanzia mwaka wa 1950, makumi ya maelfu ya wanajeshi wa Marekani wametumwa nchini Korea. Baada ya kurudi Marekani, wengi wao wamekuwa Mashahidi wenye bidii. Mara nyingi wanatuandikia barua na tunaona kwamba tulipata baraka ya kuwasaidia kiroho.
Inahuzunisha kwamba mwenzi wangu mpendwa Liz alikufa Septemba 26, 2006 (26/9/2006). Ninamkosa sana. Katika miaka 51 aliyotumika huku, alikubali kwa furaha mgawo wowote na hakulalamika kamwe. Hakupendekeza wala kudokeza kamwe turudi Marekani, nchi ambayo wakati fulani alisema kwamba hakutaka kutoka!
Ninaendelea kutumika nikiwa mshiriki wa familia ya Betheli nchini Korea. Katika miaka ya mapema, familia hiyo ilikuwa na washiriki wachache sana lakini sasa ina washiriki 250. Nina pendeleo la kutumika nikiwa mmoja wa washiriki saba wa Halmashauri ya Tawi ambayo inasimamia kazi nchini.
Korea ilikuwa nchi maskini sana tulipofika, lakini sasa ni moja ya mataifa yaliyositawi sana ulimwenguni. Kuna Mashahidi zaidi ya 95,000 nchini Korea, na asilimia 40 hivi kati yao wanatumika wakiwa mapainia wa kawaida au wasaidizi. Hizo ni kati ya sababu nyingi zinazonifanya nithamini kwamba nimeweza kumtumikia Mungu huku na kuona kundi la Mungu likikua.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Tulipofika Korea pamoja na wamishonari wenzetu
[Picha katika ukurasa wa 24]
Tukitumikia huko Pusan
[Picha katika ukurasa wa 25]
Nikiwa na Ndugu Franz katika eneo lisilo na majeshi, mwaka wa 1971
[Picha katika ukurasa wa 26]
Nikiwa na Liz muda mfupi kabla hajafa
[Picha katika ukurasa wa 26]
Ofisi ya tawi ya Korea ambako ninaendelea kutumikia nikiwa mshiriki wa familia ya Betheli