KUTOKA KATIKA HIFADHI YA VITU VYETU VYA KALE
Walisimama Imara Katika “Saa ya Jaribu”
KUANZA kwa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu mwaka wa 1914 kulifanya ulimwengu ujue hatimaye kwamba Wanafunzi wa Biblia hawaungi mkono upande wowote katika vita. (Isa. 2:2-4; Yoh.18:36; Efe. 6:12) Watumishi wa Mungu nchini Uingereza walikabili hali gani?
Kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Kijeshi ya mwaka wa 1916, wanaume waseja wenye umri wa kati ya miaka 18 na 40 walipaswa kuandikishwa jeshini. Sheria hiyo iliwaruhusu wale walio na “sababu halali za kidini au kiadili” kukataa utumishi huo. Serikali iliunda mabaraza ya mahakama ili kuamua ni akina nani ambao wangeruhusiwa kutojiunga na jeshi na kwa kiwango gani.
Baada ya muda mfupi, Wanafunzi wa Biblia wapatao 40 walifungwa katika magereza ya kijeshi, na 8 walipelekwa vitani nchini Ufaransa. Kwa sababu ya hatua hiyo isiyo ya haki, ndugu nchini Uingereza walimwandikia barua Waziri Mkuu Herbert Asquith wakilalamika kuhusu kufungwa gerezani kwa wenzao. Barua hiyo iliambatana na ombi lililotiwa sahihi na watu 500.
Kisha, taarifa zilisema kwamba ndugu wanane waliopelekwa nchini Ufaransa wamehukumiwa kupigwa risasi kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi. Lakini ndugu hao waliposimamishwa mbele ya kikundi cha wanajeshi ili wapigwe risasi, hukumu yao ilibadilishwa na hivyo wakafungwa miaka kumi gerezani. Walirudi Uingereza ili watumikie vifungo vyao katika magereza ya umma.
Vita vilipoendelea, sheria ya kuwalazimisha watu kuandikishwa jeshini iliwahusu pia wanaume waliooa. Katika kesi ya msingi iliyofanywa huko Manchester, Uingereza, mshukiwa alikuwa Henry Hudson, aliyekuwa daktari na pia Mwanafunzi wa Biblia. Mnamo Agosti 3, 1916, mahakama iliamua kwamba ana hatia, akatozwa faini, na kukabidhiwa kwa wanajeshi. Wakati huohuo, kesi nyingine ya msingi ilisikilizwa huko Edinburgh, Scotland. James Frederick Scott, kolpota aliyekuwa na umri wa miaka 25 hakupatikana na hatia yoyote. Wakili wa Serikali alikata rufani ya kesi hiyo lakini akaitupilia mbali ili ashughulikie kesi nyingine ya msingi jijini London. Pindi hiyo, ndugu anayeitwa Herbert Kipps alipatikana na hatia, akatozwa faini, na kukabidhiwa kwa wanajeshi.
Kufikia Septemba 1916, jumla ya ndugu 264 walikuwa wamejaza maombi ya kutojiunga na jeshi. Kati yao, 5 walisamehewa, 154 walipewa “kazi ya ujenzi wa taifa,” 23 wakapewa kazi za kutotumia silaha, 82 wakakabidhiwa kwa wanajeshi, na wengine wakashtakiwa kwenye mahakama za kijeshi kwa kutotii amri za kijeshi. Watu wengi walilalamikia jinsi wanaume hao walivyotendewa kikatili, na hivyo serikali ikawahamisha kutoka katika gereza la kijeshi hadi kwenye kambi za kawaida za kazi ngumu.
Edgar Clay na Pryce Hughes aliyetumika baadaye akiwa mwangalizi wa ofisi ya tawi nchini Uingereza, walifanya kazi ya kujenga bwawa huko Wales. Naye Herbert Senior, mmoja wa wale wanane waliokuwa wamerudishwa kutoka Ufaransa, alifungwa katika Gereza la Wakefield huko Yorkshire. Wengine walitumikia vifungo vyao vya kazi ngumu katika mazingira magumu sana ndani ya Gereza la Dartmoor, ambalo lilikuwa na idadi kubwa ya wafungwa waliokuwa wamekataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri zao.
Frank Platt, Mwanafunzi wa Biblia aliyekubali kufanya kazi ambazo hazihusishi kutumia silaha, aliteswa vibaya sana na kwa muda mrefu alipokataa kupigana vitani. Pia, Atkinson Padgett, aliyejifunza kweli muda mfupi tu baada ya kujiandikisha jeshini, aliteswa kikatili na wakuu wa kijeshi kwa sababu ya kukataa kupigana vitani.
Ingawa karne moja iliyopita huenda ndugu zetu hawakuelewa vizuri msimamo wetu wa Kikristo wa kutounga mkono upande wowote vitani, walitaka kumpendeza Yehova Mungu. Wale ambao majina yao yametajwa katika ripoti hii waliweka mfano bora wa kutojihusisha na vita hasa wakati huo mgumu wa “saa ya jaribu.” (Ufu. 3:10)—Kutoka katika hifadhi ya vitu vyetu vya kale nchini Uingereza.