Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Ni nini kinachothibitisha kwamba Waisraeli walishinda jiji la kale la Yeriko baada ya kulizingira kwa muda mfupi?
Kulingana na kitabu cha Yoshua 6:10-15, 20, majeshi ya Israeli yalizunguka jiji la Yeriko mara moja kila siku kwa muda wa siku sita. Siku ya saba, walizunguka jiji hilo mara saba, na Mungu akasababisha kuta imara za Yeriko zianguke. Jambo hilo liliwawezesha Waisraeli kuingia Yeriko na kulishinda jiji hilo. Je, kuna jambo lolote linalothibitisha kwamba jiji la Yeriko lilizingirwa kwa muda mfupi kama Biblia inavyosema?
Zamani, ilikuwa kawaida kwa wavamizi kuzingira jiji lenye ngome. Haidhuru kuzingirwa huko kungedumu kwa muda gani, wavamizi wangepora mali za jiji na vyakula. Hata hivyo, katika jiji la Yeriko, wachimbuaji wa vitu vya kale wamekuta chakula kingi kilichokuwa kimehifadhiwa. Kitabu kimoja kinasema hivi kuhusu jambo hilo: “Mbali na vyombo vya udongo, nafaka ndiyo iliyopatikana kwa wingi sana katika magofu. . . . Hicho ni kisa cha pekee katika historia ya vitu vya kale ya Palestina. Huenda mtungi mmoja au miwili tu ya nafaka vingeweza kupatikana, lakini kupata kiasi kikubwa hivyo cha nafaka ni jambo lisilo la kawaida.”—Biblical Archaeology Review.
Biblia inaeleza sababu iliyowafanya Waisraeli wasipore nafaka za Yeriko. Yehova aliwaamuru wasifanye hivyo. (Yos. 6:17, 18) Waisraeli walishambulia katika majira ya kuchipua, mara tu baada ya mavuno, wakati ambapo nafaka ilipatikana kwa wingi. (Yos. 3:15-17; 5:10) Hivyo basi, kupatikana kwa masalio ya nafaka nyingi katika jiji la Yeriko kunathibitisha kwamba Waisraeli walilizingira jiji hilo kwa muda mfupi, kama Biblia inavyoeleza.