Samweli Alifanya Yaliyo Sawa
Wafundishe Watoto Wako
Samweli Alifanya Yaliyo Sawa
JE, WAKATI mwingine unawaona watu wakifanya mambo mabaya?— * Samweli aliona pia jambo kama hilo. Aliishi mahali ambapo hungetarajia kuona watu wakifanya mambo mabaya. Samweli aliishi kwenye maskani ya Mungu, au mahali pa ibada katika mji wa Shilo. Acheni tuchunguze ni nini kilichomfanya Samweli aishi kwenye maskani miaka zaidi ya 3,000 iliyopita.
Kabla Samweli hajazaliwa, mama yake Hana, alitamani sana kupata mtoto. Wakati mmoja alipokuwa ametembelea maskani, Hana alisali kwa Mungu ili apate mtoto. Alisali kwa bidii sana hivi kwamba midomo yake ikaanza kutetemeka. Hilo lilimfanya kuhani mkuu Eli afikiri kwamba alikuwa amelewa. Lakini Eli alipogundua kuwa Hana alikuwa amehuzunika na hakuwa amelewa, alimbariki kwa kusema, “Mungu wa Israeli akupe ombi lako ambalo umemwomba.”—1 Samweli 1:17.
Hatimaye, Samweli alizaliwa na mama yake Hana akafurahi sana. Alimwambia mume wake Elkana hivi: ‘Nitakapoacha kumnyonyesha Samweli, nitampeleka kwenye maskani akatumikie Mungu.’ Hivyo ndivyo alivyofanya! Yaelekea wakati huo Samweli alikuwa na umri wa miaka minne au mitano hivi.
Kuhani Eli alikuwa amezeeka na wana wake Hofni na Finehasi hawakuwa wakimwabudu Yehova kwa njia inayofaa. Hata walifanya uasherati na wanawake waliotembelea maskani! Unafikiria baba yao alipaswa kufanya nini?— Bila shaka alipaswa kuwatia nidhamu na kuwakataza kufanya mambo hayo mabaya.
Kijana Samweli alikuwa akiendelea kukua na yaelekea alijua kuhusu tabia mbaya za wana wa Eli. Je, Samweli aliiga mfano wao mbaya?— Hapana. Aliendelea kufanya yaliyo sawa kama alivyokuwa amefundishwa na wazazi wake. Basi haishangazi kwamba Yehova alikasirishwa na Eli. Hata alimtuma nabii wake akiwa na 1 Samweli 2:22-36.
ujumbe kuhusu vile Yehova angeadhibu familia ya Eli, hasa vijana wake waliokuwa wabaya.—Samweli aliendelea kutumika katika maskani pamoja na Eli. Kisha usiku mmoja, Samweli alipokuwa amelala akasikia sauti ikimwita. Basi Samweli akakimbia kwa Eli, lakini Eli akamwambia kwamba hakuwa amemwita. Samweli alisikia tena sauti ikimwita mara ya pili. Baada ya kuisikia sauti hiyo mara ya tatu, Eli alimwambia Samweli ajibu hivi: “Sema, Yehova, kwa maana mtumishi wako anasikiliza.” Baada ya Samweli kujibu hivyo, Yehova akazungumza naye. Je, unajua kile ambacho Yehova alimwambia Samweli?—
Yehova alimwambia Samweli kusudi lake la kuiadhibu familia ya Eli. Asubuhi iliyofuata, Samweli aliogopa sana kumwambia Eli jambo ambalo Yehova alikuwa amemwambia. Lakini Eli alimsihi Samweli hivi: “Tafadhali usinifiche hilo.” Hivyo basi Samweli akamwambia Eli kila jambo ambalo Yehova alikuwa amesema kuwa atafanya, yaani, kama vile tu nabii wa Yehova alikuwa amemwambia Eli. Eli alijibu hivi: “Na [Yehova] afanye yaliyo mema machoni pake.” Hatimaye, Hofni na Finehasi waliuawa, naye Eli akafa pia.—1 Samweli 3:1-18.
Wakati huohuo, “Samweli akaendelea kukua, na Yehova akawa pamoja naye.” Huenda sasa Samweli alikuwa akibalehe, na hiki ni kipindi muhimu sana katika maisha ya vijana. Je, unafikiria ilikuwa rahisi kwa Samweli kuendelea kufanya yaliyo sawa hata ingawa wengine hawakufanya hivyo?— Ingawa haikuwa rahisi, Samweli alimtumikia Yehova kwa uaminifu kwa maisha yake yote.—1 Samweli 3:19-21.
Namna gani wewe? Je, unapoendelea kukua utakuwa kama Samweli? Je, utaendelea kufanya yaliyo sawa? Je, utaendelea kufuata mafundisho ya Biblia na yale ambayo umefundishwa na wazazi wako? Ukifanya hivyo, utamfurahisha Yehova na wazazi wako pia.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Kama unasoma sehemu hii pamoja na watoto, unapoona kistari kama hiki (—), tua na uwaruhusu watoe maoni yao.
Maswali:
○ Samweli alikuja kumtumikia Yehova katika maskani jinsi gani?
○ Ni hali gani ngumu ambazo Samweli alipata katika maskani?
○ Ni mfano gani ambao Samweli aliwawekea vijana?