Inamaanisha Nini Kuwa Maskini wa Kupindukia?
Inamaanisha Nini Kuwa Maskini wa Kupindukia?
UMASKINI wa kupindukia ni jambo linalotishia maisha. Unamaanisha kukosa chakula cha kutosha, maji, na fueli (yaani, kuni, makaa, mafuta, n.k.), kutia ndani makao yanayofaa, matibabu, na elimu. Umaskini unaathiri watu bilioni moja hivi, idadi ambayo ni karibu sawa na wakaaji wote nchini India. Hata hivyo, watu wengi katika maeneo kama vile Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini hawajawahi kuona mtu aliye maskini wa kupindukia. Hivyo, acheni tuone watu ambao ni maskini wa kupindukia.
Mbarushimana anaishi Rwanda, barani Afrika, pamoja na mke wake na watoto wao watano. Mtoto wao wa sita alikufa kutokana na malaria. Anasema: “Baba yetu alihitaji kugawanya shamba lake kati yetu tukiwa watoto sita. Sehemu niliyogawiwa ilikuwa ndogo sana hivi kwamba ilinilazimu kuhamishia familia yangu mjini. Mimi na mke wangu tunafanya kazi ya kubeba magunia ya mawe na mchanga. Nyumba yetu haina madirisha. Tunachota maji kwenye kisima kimoja kilicho katika kituo cha polisi. Kwa kawaida tunapata mlo mmoja kila siku, lakini wakati hakuna kazi, tunakosa chakula kwa siku nzima. Hali inapokuwa hivyo mimi huondoka nyumbani, kwa kuwa siwezi kuvumilia kuwasikia watoto wangu wakilia kwa sababu ya njaa.”
Victor na Carmen ni mafundi wa viatu. Wanaishi na watoto wao watano katika mji fulani wa mashambani nchini Bolivia. Wamekodi nyumba ndogo ya matofali ya udongo iliyochakaa. Nyumba hiyo ina paa linalovuja na haina umeme. Shule ambayo binti yao anasoma ina watoto wengi sana hivi kwamba ilimbidi Victor amtengenezee dawati ili aweze kujiunga na shule hiyo. Victor na mke wake wanatembea kilomita 10 ili kukata kuni wanazotumia kupikia chakula na kuchemshia maji ya kunywa. “Hatuna choo,” anasema Carmen. “Hivyo sisi hujisaidia kando ya mto. Pia mto huo unatumika kama mahali pa kuogea na kutupia takataka. Mara nyingi watoto wetu huwa wagonjwa.”
Francisco na Ilídia wanaishi katika eneo la mashambani la Msumbiji. Mmoja kati ya watoto wao watano wadogo alikufa kutokana na malaria baada ya hospitali kukataa kumtibu. Francisco na mke wake hupanda mpunga na viazi vitamu katika shamba lao dogo na chakula hicho kinawatosheleza kwa miezi mitatu. Francisco anasema, “Wakati mwingine mvua inakosa kunyesha au wezi wanaiba mazao yetu, hivyo mimi ninakata na kuuza mianzi inayotumika katika ujenzi, kazi
inayonisaidia kupata pesa kidogo. Pia, mimi na mke wangu tunatembea kwa muda wa saa mbili ili kukata kuni msituni. Kila mmoja wetu hubeba mzigo wa kuni—mmoja wa kupikia kwa juma zima na mwingine wa kuuza.”Watu wengi wanahisi kwamba kuna kasoro kubwa na pia ukosefu wa haki katika ulimwengu tunamoishi kwa sababu mtu 1 kati ya kila watu 7 anaishi maisha kama ya Mbarushimana, Victor, na Francisco, huku mabilioni ya wengine wakifurahia utajiri wa kupindukia. Wengine wamejaribu kurekebisha hali hiyo. Makala inayofuata inazungumzia jitihada zao na matumaini yao.
[Picha katika ukurasa wa 2, 3]
Carmen akichota maji mtoni akiwa pamoja watoto wake wawili