Je, Wajua?
Je, Wajua?
Viongozi wa dini ya Kiyahudi wa siku za Yesu walikuwa na maoni gani kuelekea watu wa kawaida?
▪ Katika karne ya kwanza W.K., viongozi wa dini na watu wenye vyeo vya juu katika jamii ya Waisraeli waliwadharau watu wenye elimu kidogo au wasio na elimu yoyote. Mafarisayo walisema hivi: “Lakini umati huu usiojua Sheria ni watu waliolaaniwa.”—Yohana 7:49.
Vitabu vingine vya marejeo vinaonyesha kwamba watu wenye vyeo waliwadharau watu wasio na elimu kwa kuwaita, ʽam ha·ʼaʹrets, au “watu wa nchi.” Mwanzoni, neno hilo lilikuwa jina la heshima kwa raia wa eneo hususa. Halikutumiwa tu kuwarejelea watu wa hali ya chini, bali pia watu mashuhuri.—Mwanzo 23:7; 2 Wafalme 23:35; Ezekieli 22:29.
Hata hivyo, kufikia siku za Yesu, neno hilo lilitumiwa kuwarejelea watu wasiojua Sheria ya Musa au walioshindwa kufuata mambo madogo-madogo ya mapokeo ya marabi. Mishna (mkusanyo wa maandishi mbalimbali yaliyotumiwa kuandika Talmud) inaonya kuhusu kulala katika nyumba za ʽam ha·ʼaʹrets. Kulingana na kitabu kimoja cha marejeo, (The Encyclopedia of Talmudic Sages), Rabbi Meir, msomi wa karne ya pili alifundisha: “Mtu akimwoza binti yake kwa am ha’aretz, ni kana kwamba anamfunga na kumweka mbele ya simba anayekanyanga windo lake kabla ya kulinyafua.” Talmud inamnukuu rabi mwingine aliyesema kwamba “watu wasio na elimu hawatafufuliwa.”
Jina Kaisari lina maana gani kama linavyotumiwa katika Biblia?
▪ Kaisari lilikuwa jina la familia ya Kiroma ya Gayo Yulio Kaisari, aliyeteuliwa kuwa dikteta wa Roma mwaka wa 46 K.W.K. Maliki kadhaa Waroma walichagua jina hilo, kutia ndani watatu wanaotajwa kwa jina katika Biblia—Augusto, Tiberio, na Klaudio.—Luka 2:1; 3:1; Matendo 11:28.
Tiberio aliwekwa kuwa maliki mwaka wa 14 W.K., na alitawala kipindi chote cha huduma ya Yesu duniani. Yeye ndiye Kaisari aliyekuwa mamlakani wakati Yesu aliposema maneno haya ili kujibu swali kuhusu ulipaji wa kodi: “Mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari, lakini Mungu vitu vya Mungu.” (Marko 12:17) Yesu hakumaanisha kwamba jina Kaisari lilipaswa kutumiwa tu kumrejelea Tiberio. Badala yake, jina “Kaisari” lilifananisha wenye mamlaka au Serikali.
Mnamo mwaka wa 58 W.K., Festo alijaribu kumhukumu mtume Paulo isivyo haki ili awafurahishe Wayahudi, lakini mtume huyo akatumia haki yake akiwa raia wa Roma kukata rufani kwa Kaisari. (Matendo 25:8-11) Kwa kufanya hivyo, Paulo hakuwa akiomba ahukumiwe na Nero mwenyewe, aliyekuwa maliki wakati huo, bali na mahakama kuu zaidi ya miliki hiyo.
Jina Kaisari, ambalo lilikuwa la kifamilia, lilihusianishwa sana na utawala hivi kwamba hata baada ya utawala wa familia ya Kaisari kwisha, jina hilo liliendelea kutumiwa kuwarejelea watawala.
[Picha katika ukurasa wa 29]
Dinari ya fedha yenye picha ya Tiberio