Je, Wajua?
Mawe ya kusaga ya mkononi yalitumiwaje nyakati za kale?
Mawe ya kusaga ya mkononi yalitumiwa kusaga nafaka kuwa unga ili kutengeneza mkate. Mwanamke au watumishi walitumia mawe hayo kila siku kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Sauti ya jiwe la kusaga ilihusianishwa na maisha ya kila siku katika nyakati za kale.—Kutoka 11:5; Yeremia 25:10.
Michoro na sanamu kutoka Misri ya kale zinaonyesha jinsi mawe hayo yalivyotumiwa. Nafaka iliwekwa juu ya jiwe lililobonyea kidogo, lenye uso bapa ambalo nyakati fulani liliitwa tandiko la farasi. Anayesaga unga angepiga magoti mbele ya jiwe hilo huku akiwa ameshika kwa mikono yake jiwe dogo la kusagia, ambalo angetumia kusaga nafaka zilizo juu ya jiwe hilo. Kulingana na chanzo kimoja, jiwe hilo la kusaga lingekuwa na uzito kati ya kilogramu 2 na 4. Ikiwa jiwe hilo lingetumiwa kama silaha, lingeweza kusababisha kifo.—Waamuzi 9:50-54.
Kusaga nafaka kulikuwa muhimu sana ili kuitunza familia hivi kwamba sheria ya Biblia ilikataza kuchukua mawe ya kusagia kuwa rehani. Andiko la Kumbukumbu la Torati 24:6 linasema hivi: “Mtu yeyote asitwae kuwa rehani jiwe la kusagia la mkononi au jiwe lake la juu la kusagia, kwa sababu ni nafsi anayoitwaa kuwa rehani.”
Usemi “kifuani pa” unarejelea nini?
Biblia inasema kwamba Yesu yuko “kifuani pa Baba.” (Yohana 1:18) Usemi huo unarejelea kibali na uhusiano wa karibu ambao Yesu anao pamoja na Mungu. Usemi huo ulitokana na desturi iliyofuatwa na Wayahudi wakati wa mlo.
Katika siku za Yesu, Wayahudi waliketi katika makochi yaliyopangwa kuzunguka meza ya chakula. Kila mlaji aliketi kwa kujilaza huku akitazama kuelekea mezani na kuweka miguu yake nyuma, wakati huo akiegama kwenye mto wa kochi kwa kiwiko cha mkono wake wa kushoto. Kukaa hivyo kulifanya mkono wa kulia uwe huru. Kwa kuwa, walaji wote waliketi kwa kujilaza upande wa kushoto kwa ukaribu, chanzo kimoja kinasema, “kichwa cha mtu mmoja aliye jirani kingekuwa karibu na kifua cha mtu aliyekaa nyuma yake na hivyo ingeweza kusemwa kwamba yuko ‘kifuani pa’ mtu mwingine.”
Kuwa katika kifua cha kichwa cha familia au mkuu wa karamu, kulionwa kuwa heshima ya pekee au pendeleo. Hivyo, katika Pasaka ambayo Yesu alihudhuria kwa mara ya mwisho, mtume Yohana, yule “mwanafunzi ambaye Yesu alikuwa akimpenda,” aliketi kifuani pa Yesu. Hivyo, Yohana angeweza ‘kuegemea nyuma kifuani pa Yesu’ ili kumuuliza swali.—Yohana 13:23-25; 21:20.