Je, Wajua?
Herode alikabili changamoto gani alipokuwa akijenga hekalu la Yerusalemu?
Mwanzoni, Sulemani alijenga hekalu la Yerusalemu juu ya mlima na akaagiza kuta zijengwe upande wa mashariki na magharibi ili kutengeneza mfululizo wa ngazi pana kuzunguka hekalu hilo. Herode alitaka kujenga hekalu zuri zaidi ya lile la Sulemani, kwa hiyo akaanza kurekebisha na kupanua hekalu lililokuwapo.
Mafundi wa Herode walipanua eneo tambarare kaskazini mwa hekalu ili kuongeza mfululizo wa ngazi pana katika eneo hilo. Eneo tambarare lenye upana wa meta 32 liliongezwa upande wa kusini. Walitengeneza safu ya vyumba vya mawe na ukuta mnene kuzunguka vyumba hivyo. Katika sehemu fulani, ukuta huo ulifikia urefu wa meta 50.
Herode alijitahidi asiwakwaze Wayahudi au kuvuruga shughuli zilizokuwa zikiendelea hekaluni. Mwanahistoria Myahudi Yosefo anasema kwamba Herode aliwafundisha makuhani wa Kiyahudi kuchonga mawe na useremala kwa kuwa wao tu ndio walioruhusiwa kuingia katika sehemu takatifu za hekalu.
Herode alikufa kabla ya mradi huo kukamilika. Kufikia mwaka wa 30 W.K., hekalu hilo lilikuwa limejengwa kwa miaka 46. (Yohana 2:20) Kitukuu cha Herode, Agripa wa Pili, alimaliza kazi hiyo katikati ya karne ya kwanza W.K.
Kwa nini watu wa Malta walifikiri kwamba mtume Paulo alikuwa muuaji?
Huenda baadhi ya watu wa Malta waliathiriwa na mafundisho ya dini ya Wagiriki. Fikiria kilichotokea baada ya meli aliyopanda Paulo kuvunjika akiwa Malta, kama inavyosimuliwa katika kitabu cha Matendo. Mtume huyo alipokusanya kuni na kuziweka juu ya moto ili kuwapasha joto abiria wenzake, nyoka-kipiri alijifunga kwenye mkono wake. Walipoona hilo, wenyeji wa kisiwa hicho walisema hivi: “Hakika mtu huyu ni muuaji, na ingawa alifika mahali salama kutoka baharini, haki yenye kudai kisasi haikumruhusu aendelee kuishi.”
Neno la Kigiriki “Haki” lililotumika hapa ni “di’ke.” Neno hilo linaweza kumaanisha haki katika hali isiyo halisi. Hata hivyo, kulingana na hekaya za Kigiriki, mungu wa kike wa haki aliitwa Dike. Ilidhaniwa kwamba alisimamia mambo yote ya wanadamu na alitoa taarifa kwa Zeu kuhusu ukosefu wowote wa haki ambao haukugunduliwa ili wenye makosa waadhibiwe. Hivyo, kulingana na chanzo kimoja, huenda wenyeji wa Malta walifikiri hivi: “Ingawa Paulo hakufa baharini, ametiwa alama na sasa anahukumiwa na mungu wa kike Dike . . . kupitia nyoka kipiri.” Watu walibadili maoni yao walipoona Paulo yuko hai.