Mambo Saba Muhimu ya Kuhakikisha Chakula Ni Salama na Chenye Lishe
Kwa nini ni muhimu kuhangaikia unachokula
Ili uwe na afya nzuri, sehemu fulani inategemea unakula nini. Ukihakikisha chakula chako ni salama na unakula chakula chenye lishe, unaweza kuboresha afya yako. Tofauti na hilo, usipohangaikia usalama wa chakula chako na ukila chakula kisicho na lishe, unaweza kujisababishia matatizo makubwa ya afya, kama vile mafuta yasiyofaa yanavyoweza kulisababishia gari matatizo. Huenda matatizo hayo yasionekane mara moja, lakini lazima yatajitokeza.—Wagalatia 6:7.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linasema kwamba “kila nchi ulimwenguni huathiriwa na aina moja au zaidi za utapiamlo”—neno linalotumiwa kuonyesha si ukosefu wa chakula chenye lishe tu bali pia hali kama vile kuwa wanene kupita kiasi. Kutumia mara nyingi vyakula na vinywaji visivyo na lishe huongeza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo, kiharusi, kisukari, na kansa. Kulingana na uchunguzi mmoja, kula chakula kisicho na lishe kulisababisha vifo milioni 11 katika mwaka mmoja hivi karibuni. WHO inakadiria kwamba chakula chenye sumu hutokeza vifo vya zaidi ya watu elfu moja kila siku na kuwasababishia mamia ya mamilioni ya watu matatizo ya afya.
Biblia inatutia moyo kuchukua mambo hayo kwa uzito. Inatufundisha kwamba Mungu ndiye “chanzo cha uhai.” (Zaburi 36:9) Uhai ni zawadi, na tunaonyesha uthamini kwa kutunza afya yetu na ya familia zetu. Fikiria jinsi unavyoweza kufanya hivyo.
Mambo manne ya kuhakikisha chakula ni salama
1. Tayarisha chakula kwa njia salama.
Kwa nini? Viini a hatari vilivyo katika chakula na maji yaliyochafuliwa vinaweza kuingia mwilini mwako na kukufanya kuwa mgonjwa.
Wataalamu wa afya wanapendekeza:
Kabla ya kutayarisha chakula, nawa mikono ukitumia maji na sabuni. b Sugua mikono yako kwa angalau sekunde 20. Sugua upande wa nyuma wa mikono na pia katikati ya vidole vyako na chini ya kucha. Suuza na ukaushe mikono vizuri.
Tumia maji na sabuni kuosha mbao unazotumia kukatia vyakula, vyombo, na chochote kingine kinachogusa chakula. Isitoshe, epuka kutumia ubao uleule kukatia chakula kitakachopikwa na ambacho hakitapikwa.
Osha matunda yote na mboga, pia ni muhimu kutumia dawa ya kuua viini ikiwa unaishi katika eneo ambalo mimea inaweza kuwa imenyunyiziwa maji yaliyochafuliwa na kinyesi.
2. Usiweke vyakula ambavyo havijapikwa na vilivyopikwa.
Kwa nini? Viini kutoka kwenye vyakula ambavyo havijapikwa kama vile nyama na umajimaji wake vinaweza kuchafua vyakula vingine.
Wataalamu wa afya wanapendekeza:
Tenganisha vyakula ambavyo havijapikwa—hasa nyama—na vyakula vilivyo tayari kuliwa unapovibeba kutoka sokoni na unapovihifadhi.
Baada ya kukata nyama mbichi, nawa mikono yako kabisa, safisha kisu na ubao uliotumia kukatia kabla ya kukata chakula kingine chochote.
3. Hakikisha kwamba chakula kinachohitaji kupikwa kinaiva vizuri.
Kwa nini? Viini hatari huuawa wakati tu chakula kinafikia kiwango kinachofaa cha joto.
Wataalamu wa afya wanapendekeza:
Pika chakula hadi kinapokuwa moto sana. Kwa angalau sekunde 30, chakula, kutia ndani, sehemu za ndani kabisa za nyama, zinapaswa kupigwa na joto la digrii 70 Selsiasi.
Hakikisha supu na michuzi inachemka.
Unapotaka kula masalio, hakikisha unayapasha hadi yanapokuwa moto kabisa na kutokeza mvuke.
4. Hifadhi chakula katika kiwango cha joto kinachofaa.
Kwa nini? Chakula kinapohifadhiwa katika hali-joto ya kati ya digrii 5 na 60 Selsiasi kwa dakika 20 tu, idadi ya bakteria inaweza kuongezeka mara mbili. Mbali na hilo, nyama mbichi isipohifadhiwa katika viwango vya joto vinavyofaa, bakteria fulani wanaweza kutokeza sumu ambazo haziwezi kuangamizwa kwa kupika.
Wataalamu wa afya wanapendekeza:
Dumisha chakula kikiwa moto au baridi, si kikiwa vuguvugu, ili kupunguza au kuzuia viini visiongezeke.
Usiache chakula nje kwa zaidi ya saa mbili. Ikiwa chumba kina joto la zaidi ya digrii 32 Selsiasi, usiache chakula nje kwa zaidi ya saa moja.
Baada ya kupika, dumisha joto la chakula hadi kabla tu ya kukiandaa mezani.
Mambo matatu muhimu ya kula chakula chenye afya
1. Kula aina mbalimbali za matunda na mboga kila siku.
Matunda na mboga ni chanzo muhimu cha vitamini, madini, na vitu vingine ambavyo ni muhimu ili kuwa na afya nzuri. WHO inasema kwamba mwili wako unahitaji angalau sehemu tano ya matunda na mboga kila siku. Visehemu hivyo havipaswi kuwa na mizizi yenye wanga, kama vile viazi au viazi vitamu.
2. Kula kiasi kidogo tu cha mafuta.
WHO inapendekeza ule kiasi kidogo sana cha vyakula vilivyokaangwa na vyakula vilivyowekwa kemikali ya kuzihifadhi au vilivyookwa ambavyo mara nyingi vina mafuta hatari kwa afya. Inapowezekana, tumia mafuta yasiyo kifu ya mboga unapopika. c Mafuta hayo ni mazuri zaidi kuliko yale yaliyo kifu.
3. Dhibiti kiasi cha chumvi na sukari unachokula.
WHO inapendekeza kwamba watu wazima wasitumie chumvi inayozidi kijiko kidogo cha chai kwa siku. Pia, WHO inapendekeza kiasi cha sukari kisizidi milimeta 60 (vijiko 12 vya kawaida) kwa siku. d Sukari ndicho kiungo kikuu katika vyakula na vinywaji vingi vilivyotayarishwa viwandani. Kwa mfano, kinywaji kama vile soda ya milimeta 355 inaweza kuwa na milimeta 50 (vijiko 10 vidogo) vya sukari. Licha ya kwamba vinjwaji kama hivyo huwa na kalori nyingi sana, havisaidii mwili kupata lishe kwa njia yoyote.
Biblia inasema: “Mtu mwerevu huona hatari na kujificha, Lakini wajinga husonga mbele na kupata madhara.” (Methali 22:3) Ukitenda kwa werevu kuhusiana na mazoea yako ya kula na kufanya mabadiliko yanayohitajika, utamwonyesha Mungu kwamba unathamini uhai na afya yako.
Maoni yasiyo sahihi
Uwongo: Chakula ni salama ikiwa mwonekano, harufu, na ladha yake iko sawa.
Ukweli: Bakteria bilioni 10 wanapojikusanya ndipo maji ya lita moja yanaweza kutokeza rangi nzito, lakini bakteria 15 hadi 20 tu ni hatari kiasi cha kukufanya kuwa mgonjwa. Ili kuhakikisha kwamba chakula na vinywaji vyako ni salama, fuata maagizo ya kiwango cha joto na muda ulioonyeshwa wa kuandaa, kula, na kuhifadhi.
Uwongo: Nzi hawachafui chakula.
Ukweli: Nzi hula na kuzaliana katika uchafu kama vile kinyesi, kwa hiyo, mara nyingi miguu yao hubeba mamilioni ya viini vinavyoweza kusababisha magonjwa. Ili kulinda chakula kilichotayarishwa kisichafuliwe na nzi, kifunike kabisa.
Uwongo: “Nimekuwa nikila chakula kisicho na lishe kwa muda mrefu hivi kwamba hakuna faida hata nikibadili mazoea yangu ya kula.”
Ukweli: Wataalamu wamegundua kwamba kula chakula chenye lishe sasa kutapunguza uwezekano wa kufa mapema na kwamba utapata manufaa mengi kadiri unavyoendelea kula chakula chenye lishe.
a Viini, au vijidudu, ni viumbe vidogo sana ambavyo haviwezi kuonekana bila kutumia hadubini. Vinatia ndani bakteria, virusi, na vimelea. Vijidudu fulani vina manufaa mwilini, lakini vile hatari vinaweza kukuumiza au hata kukuua.
b Maji na sabuni huondoa viini zaidi kuliko maji peke yake.
c Mafuta yasiyo kifu huendelea kuwa majimaji hata katika hali ya joto ya kawaida, wala hayagandamani.
d Aina ya sukari inayotajwa hapa inatia ndani sukari iliyotayarishiwa kiwandani, kama vile sukari inayotumiwa kwenye chai, asali ya nyuki, asali ya matunda, na maji ya matunda. Hilo halitii ndani sukari ya asili inayopatikana katika matunda, mboga, na maziwa.