ENDELEA KUKESHA!
Je, kuna tumaini lolote kwamba mashambulizi hayo yatakwisha?
Katika mwezi wa Julai 2022, mashambulizi ya kikatili ya bunduki yalitokea kotekote ulimwenguni:
“Nchini Japani kuuawa kwa mwanasiasa maarufu [Shinzo Abe aliyekuwa Waziri Mkuu hapo awali] kulileta mshtuko ndani ya nchi hiyo na ulimwenguni pote, hasa kwa sababu nchi hiyo ina kiwango kidogo tu cha uhalifu na pia ina sheria kali zinazodhibiti matumizi ya bunduki.”—Julai 10, 2022, The Japan Times.
“Kuna mshtuko mkubwa nchini Denmark baada ya mwanamume mwenye bunduki kuwaua watu watatu waliokuwa wakifanya ununuzi kwenye duka moja jijini Copenhagen.”—Julai 4, 2022, Reuters.
“Afrika Kusini: Watu 15 waliuawa baada ya wanaume wenye bunduki kushambulia baa moja katika mji wa Soweto.”—Julai 10, 2022, The Guardian.
“Zaidi ya watu 220 waliuawa katika mashambulizi ya bunduki yaliyofanyika Marekani katika mwisho juma wa sherehe za Julai 4.”—Julai 5, 2022, CBS News.
Je, kuna tumaini lolote kwamba mashambulizi kama hayo yatakwisha? Biblia inasema nini?
Ukatili Utakwisha
Biblia inafafanua kipindi tunachoishi kuwa “siku za mwisho,” kipindi ambacho watu wangekuwa wakali na wakatili sana. (2 Timotheo 3:1, 3) Matendo hayo ya kikatili huwafanya watu kuishi kwa hofu. (Luka 21:11) Hata hivyo, Biblia inaahidi kwamba ukatili utakwisha na ‘watu watakaa katika makao ya kudumu yenye amani, katika makao salama na mahali pa kupumzika penye utulivu.’ (Isaya 32:18) Ukatili utakwisha jinsi gani?
Mungu atawaangamiza waovu na kuharibu silaha zote.
“Lakini waovu, wataangamizwa kutoka duniani.”—Methali 2:22.
“[Mungu] anakomesha vita katika dunia yote. Anauvunja upinde na kuuvunja mkuki vipandevipande; anayateketeza magari ya vita motoni.”—Zaburi 46:9.
Mungu ataondoa mizizi ya ukatili kwa kuwafundisha watu kuishi kwa amani.
“Hawatasababisha madhara yoyote wala uharibifu wowote katika mlima wangu wote mtakatifu, kwa maana kwa hakika dunia itajaa ujuzi kumhusu Yehova kama maji yanavyoifunika bahari.”—Isaya 11:9.
Hata sasa, Mungu anawafundisha watu ulimwenguni pote kuepuka ukatili na kuacha kutumia silaha, yaani, ‘kufua panga zao ziwe majembe ya plau na mikuki yao iwe miundu.’—Mika 4:3.
Ili ujifunze mengi zaidi kuhusu ahadi ya Biblia ya ulimwengu usio na chuki, soma makala yenye kichwa, “Je, Inawezekana Kuishi Bila Woga?”
Ili ujifunze mengi zaidi kuhusu suluhisho la kudumu la tatizo la ukatili, soma makala yenye kichwa, “Hatimaye Amani Duniani!”