Visiwa Solomoni
Visiwa Solomoni
TAIFA la Kimelanesia la Visiwa Solomoni, liitwalo kwa upendo “Visiwa vyenye Furaha,” limeenea kama mikufu miwili ya lulu yenye thamani katika bahari ya Pasifiki yenye rangi ya feruzi mahali-mahali. Mkururo huo wa jozi ya visiwa vya volkano na vya matumbawe huanzia Kisiwa-Matumbawe cha Ontong Java kusini kidogo tu mwa Ikweta, ukipakana na Papua New Guinea upande wa magharibi na kuenea kwa yapata kilometa 1,500 kuelekea kusini-mashariki hadi Visiwa Santa Cruz, vinavyotia ndani Visiwa Reef vilivyoko karibu na Vanuatu ambacho ni jirani upande wa kusini. Visiwa vingi kati ya kikundi cha visiwa Solomoni vimefunikwa na misitu iliyositawi sana na mfululizo wa miamba iliyochongoka na vilima imara vya mbavuni vinavyofanyiza safu za milima, kukiwa na mabonde membamba yenye vina virefu kati yavyo. Ikiwa na jumla ya eneo la kilometa za mraba zipatazo 27,000, nchi hiyo iliyo peke yayo ni ya pili kwa ukubwa, kufuatia Papua New Guinea kati ya mataifa ya visiwa vya Pasifiki Kusini.
Mvumbuzi wa kwanza kutoka Ulaya kufika kwenye fuko hizo nyeupe alikuwa Álvaro de Mendaña, baharia Mhispania, katika 1568. Alikuwa akitafuta ile migodi ya dhahabu ya kihekaya iliyopotea ya Mfalme Sulemani; badala yake alivumbua vile alivyoviita Visiwa Solomoni (Sulemani), lakini hapakuwa na dhahabu, isipokuwa ile dhahabu ipatikanayo kwenye matope ya mito katika Guadalcanal.
Watu wa Jamii Mbalimbali Wenye Jambo Moja Linalofanana
Visiwa hivyo ni makao ya watu wa jamii mbalimbali wapatao 300,000 walio na rangi ya ngozi kuanzia buluu-nyeusi hadi hudhurungi nyangavu, wakiwa na nywele zinazotofautiana
kuanzia mashungi yaliyofumwa kwa kukazwa, yenye misokoto miangavu ya kimanjano hadi zile nyekundu nyangavu za Wamelanesia wengi, ambazo hutofautiana kwa kupendeza na zile nywele laini, nyeusi zilizonyooka za Wapolinesia. Katika Visiwa Solomoni watu huwasiliana katika lugha nyingi, kukiwa na lugha na lahaja zaidi ya 90 zinazozungumzwa huko. Hata hivyo, watu wengi hutumia Kiingereza au Kipidgini cha Kimelanesia na Kiingereza wanapozungumza na majirani kutoka vikundi vya visiwa na makabila tofauti.Wapolinesia huishi katika visiwa vya mbali vya Ontong Java, Rennell, Bellona, Sikaiana katika Visiwa Stewart, na Tikopia na Anuta katika Visiwa Santa Cruz. Vikundi vikubwa vya Wamaikronesia kutoka Kiribati wamekusanyika na kufanya makao katika visiwa Wagina na Gizo magharibi mwa Solomoni, pamoja na katika Honiara, jiji kuu la Guadalcanal.
Mbali na uraia wao wa Visiwa Solomoni, jambo moja linalofanana kwa watu hao wenye kutofautiana ni kupendezwa kwa kina kirefu kuelekea Biblia. Watu hao wapenda dini sana, huonea shangwe kuimba kwa bidii nyimbo za dini katika kanisa la kijijini mwao, ambalo wao huhudhuria mara kadhaa kwa juma, wengine wao hata kila siku. Unabii wa Biblia huwavutia sana, hasa ule wa vitabu vya Danieli na Ufunuo. Wao huitikadi kwa uthabiti kuwa kwa kweli tunaishi katika siku za mwisho za mfumo huu wa kale. Itikadi hiyo huwafanya, kwa msingi, wawe watu ambao ni rahisi sana kuzungumza nao juu ya ahadi za Yehova Mungu kuleta amani na furaha ya kudumu kupitia Ufalme wake wa kimbingu.
Visiwa Vyenye Furaha Vyasikia juu ya “Mungu Mwenye Furaha”
Ile “habari njema ya Mungu mwenye furaha” imehubiriwa kwa bidii kotekote katika visiwa sita kati ya vile vikuu na katika visiwa vingi vidogo zaidi tangu 1953. (1 Tim. 1:11, NW) Katika miaka hiyo ya mapema, uangalizi wa kazi ya kueneza evanjeli katika Visiwa Solomoni ulikuwa ukifanywa na tawi la Australia la Watch Tower Society na kisha na tawi la Papua New Guinea. * Mashahidi wajasiri kutoka Papua New Guinea, kama vile John Cutforth, R. L. (Dick) Stevens, Les Carnie, na Ray na Dorothy Paterson, walizuru idadi yenye kuongezeka ya ndugu na dada vichakani. Mara nyingi waliishi nao katika nyumba zao za majani zenye paa na kuta zilizotengenezwa kwa majani bapa ya mivumo. Katika Aprili 18, 1977, shirika la Jehovah’s Witnesses of the Solomon Islands Trust Board lilianzishwa kisheria, likifungua njia kwa ajili ya mpanuko zaidi na kupanga kitengenezo kazi ya kuhubiri kwa urahisi zaidi.
Katika Julai 1978 Visiwa Solomoni vilijipatia uhuru wa kisiasa. Ndugu walifurahi kuwa shirika la kwao, Jehovah’s Witnesses of the Solomon Islands Trust Board Inc., lilikuwa tayari limesajiliwa kabla ya badiliko hilo la serikali, kwa kuwa vizuizi viliwekwa baadaye dhidi ya kuingiza dini mpya katika
eneo hilo. Iliamuliwa kwamba Visiwa Solomoni viwe na ofisi ya tawi yavyo vyenyewe ili kupanua hata zaidi kazi ya kuhubiri katika hivyo “visiwa vyenye furaha.” Punde baada ya uamuzi huo kufanywa, Glenn Finlay kutoka tawi la Papua New Guinea aliwasili huko pamoja na mke wake, Merlene, kwa ajili ya kuratibu kazi hiyo.Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Ndugu Finlay kufika kwenye Visiwa Solomoni. Licha ya kutumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko na wa wilaya katika pindi tofauti-tofauti, katika 1965 alitumia miezi mitatu katika Malaita kaskazini akiwa painia wa pekee aliyepewa mgawo na tawi la Papua New Guinea.
Ofisi ya Tawi ya Kwanza
“Ofisi yetu ya tawi ya kwanza ilianzishwa katika chumba cha chini ya ardhi cha nyumba ya Bob Seccombe katika Kilele cha Lengakiki, Honiara,” aandika ndugu Finlay kuhusu mwaka 1978. Chumba hicho kidogo cha chini ya ardhi kilikuwa tayari kimefanyiza historia ya kitheokrasi. Kilitumika kuwa Jumba la Ufalme la kwanza katika kisiwa Guadalcanal na baadaye kuwa bohari ya fasihi ya kwanza katika Visiwa Solomoni. Na kwa vile Ndugu Seccombe aliandaa nyumba ndogo ya orofa yenye chumba kimoja cha kulala iliyokuwa nyuma ya jengo, nyumba yake pia ilitumika ikiwa Betheli ya kwanza.
Ndugu Finlay aendelea kueleza hivi: “Tulianza tukiwa na taipureta moja tu ya kupigwa kwa mikono na mashine moja ya kurudufisha yenye kuendeshwa kwa mikono, lakini tulikuwa na mandhari nzuri sana ya maji-buluu ya mlango-bahari.” Karibu
miaka 50 iliyopita, katika Novemba 13, 1942, mlango-bahari huo ulikuwa ndipo mahali pa mojawapo mapigano makali zaidi katika historia ya manowari. Waamerika wakaja kuiita Mlangobahari Sakafu ya Chuma, msimbo wa jina uliotokana na idadi ya meli zilizokuwa zikishika kutu chini ya uso wao.Baada ya miaka 30 ya utumishi, Ndugu Seccombe na mkewe Joan, walirudi Australia kwa sababu za kiafya. Ingawa hawakupata watoto wao wenyewe, idadi isiyohesabika ya watoto wao na wajukuu wa kiroho huthamini sana utumishi wao wenye upendo.
Acheni turudi kwenye ripoti ya Ndugu Finlay: “Denton Hopkinson na mkewe waliwasili toka Ufilipino katika 1978. Kwa ndugu wengi, yeye alikuwa ndiye mwangalizi wa eneo la dunia wa kwanza waliyepata kuona. Katika miaka michache iliyofuata iliona ujenzi wa ofisi ya tawi ya ghorofa mbili na Makao ya Betheli.” Lo! huo ulikuwa mradi ulioje! Ndugu na dada katika Honiara walichimbua vipande vikubwa-vikubwa vyenye ncha kali sana kwa kutumia vyombo vya mikononi tu. Ingawa ujenzi wa tawi ulikuwa shughuli ngumu na ya muda mrefu, ukichukua karibu miaka mitatu, ulikuwa pia ni wonyesho mkuu wa upendo wa Kikristo. Na kama bakshishi ya ziada, baadhi ya wafanyakazi waliovutwa kuja kwenye eneo la ujenzi wangemtumikia Yehova baadaye katika njia nyingine za pekee.
Ndugu kumi vijana walikuja kufanya kazi wakati wote kwenye eneo la ujenzi chini ya mwelekezo wa Rodney Fraser, mmojawapo washiriki wa Halmashauri ya Tawi, ambaye pia alikuwa mjenzi. Wengi wa wale waliojitolea walitoka katika makutaniko yaliyokuwa vichakani. Kwa hiyo, walikuwa bado hawajawahi kutumia zana za ujenzi hapo mbeleni. Hata hivyo, baada ya miaka mitatu ya kufanya kazi na Ndugu Fraser na idadi fulani ya ndugu wengine kutoka Australia, hawakuwa tu wamekuza stadi thabiti za ujenzi bali pia walithamini sana jinsi tengenezo la Yehova la kidunia linavyotenda kazi na walipata ustadi bora zaidi katika kutoa habari njema kwa wengine.
Saba kati ya wale vijana waliendelea kuongeza utumishi wao
kwa Yehova katika njia moja au nyingine. Omega Nunu alirudi nyumbani kwao katika kijiji cha Taba’a kilichoko juu kwenye sehemu ya milima ya Malaita wanakokaa Wakwara’ae. Yeye akawa mzee peke yake katika kutaniko. Lilio Liofasi alibaki kwa miaka minane akiwa mojawapo washiriki wa kwanza wa familia ya Betheli. Sasa yeye hutumikia akiwa pamoja na mkewe, Priscilla, mzawa wa Ufilipino, katika sehemu nyingine ya utumishi wa wakati wote. Ndugu wawili wa kimwili, Joe Kwasui na David Kirite’e, waliopata kuwa maseremala, waliingia pia katika utumishi wa wakati wote. Walishiriki katika kuleta kweli kwenye Visiwa Santa Cruz mashariki mwa Visiwa Solomoni. Billy Kwalobili, aliyepata kuwa stadi katika kulaza vigae, alitumikia akiwa painia wa pekee katika Ndeni, kisiwa kilicho kikubwa zaidi katika Visiwa Santa Cruz, na sasa anafanya upainia katika Visiwa Reef vya mbali. Pedro Kanafiolo, ndugu mwenye nguvu na nishati kutoka Malu’u kaskazini mwa Malaita anatumikia sasa akiwa painia wa pekee katika eneo jipya kwa kulinganisha kwenye kisiwa San Cristobal. Simon Maedalea, aliyetoka kwenye mradi wa tawi akiwa seremala, alifanya upainia baadaye katika Malaita mashariki. Ndugu hao wenye bidii na nishati wamekuwa kwenye mstari wa mbele katika kazi ya kuhubiri kwenye “Visiwa Vyenye Furaha” vilivyotawanyika.Mikusanyiko—Matukio Makubwa Yenye Shangwe
Mikusanyiko ilikuwa matukio makubwa yenye shangwe, kila mmoja ukihitaji matayarisho mengi. Kila hotuba na drama ilipaswa kutafsiriwa kwa Kipidgini cha Visiwa Solomoni. Kisha drama hizo zilipaswa kunaswa tena kwenye utepe, kwa kutumia sauti za Mashahidi wa Honiara huku muziki na sauti ikiongezwa kutoka kwa kanda za Kiingereza. Baada ya saa nyingi za kazi, tepe hizo zilipelekwa zikiwa katika umbo la kaseti kwa ajili ya kutumika katika mazoezi. Ndugu na dada walijizoeza kwa kutumia tepu-rekoda ndogo zenye kutumia betri, katika mwangaza hafifu kwenye Majumba ya Ufalme madogo yaliyoezekwa makuti. Mikusanyiko mengine yalikuwa madogo sana hivi kwamba hakukuwa na waigizaji wa kutosha kuwekwa katika drama
hizo. Kwa hiyo katika drama fulani, slaidi kutoka Ulaya zilionyeshwa pamoja na kanda hizo. Akina ndugu katika sehemu hizo za mbali walisisimka kuona masimulizi hayo ya Biblia!Karibu na mwisho wa 1979, visiwa viwili vilitumiwa kwa ajili ya mkusanyiko mmoja mdogo kwenye Visiwa Santa Cruz. Ili wajumbe waweze kuona utoaji wa slaidi wa drama, hadhirina nzima ililazimika kuhama kutoka kwenye kisiwa kidogo ambapo vipindi vingi vilikuwa vimefanywa hadi kwenye kingine kikubwa zaidi kilichokuwa na nguvu za umeme zifaazo kwa projekta ya slaidi. Wazia ukitazama umati huo wenye uchangamfu na msisimuko ukisafiri kuvuka bahari katika mitumbwi ya kuchongwa kwenda kujaza jumba pomoni, huku watazamaji waliopendezwa wakisongamana kuchungulia kupitia kila dirisha! Kisha walipiga makafi kurudi kwa furaha, wakitafakari chini ya mbalamwezi mwangavu wavukapo bahari hiyo yenye kumetameta, yenye maji mawewa (safi sana). Ungaliweza kuachwa na kumbukumbu isiyoweza kusahaulika kamwe.
Habari Njema Zaenea
Kwa miaka mingi utendaji wa kuhubiri uliendeshwa katika visiwa viwili tu, Malaita na Guadalcanal, ambavyo vilikuwa na kutaniko moja tu. Katika miaka ya 1960 na 1970, vikundi vidogo vya watu wanaopendezwa viliundwa katika Munda na Gizo magharibi mwa Visiwa Solomoni. Lakini maendeleo yalikuwa ya polepole. Hatimaye, kupendezwa kulienea katika sehemu nyingine kadiri mapainia walivyosafiri hadi Choiseul upande wa magharibi na Visiwa Santa Cruz katika vikundi vya visiwa vya mashariki vilivyo nje zaidi.
Malaita ni maarufu kwa mambo mawili: la kwanza, hiyo ni chimbuko la pesa za kauri (simbi) zilizotumiwa kulipia mahari; na la pili, hiyo ni makao ya watu wenye maungo, wenye tamaa kubwa ya kusafiri. Wamalaita ni wafanyakazi wenye bidii, wengi wao wakiwa wanadumisha mashamba ya milimani yenye ukubwa wa kusifika kwelikweli. Kwa sababu ya tabia yao ya kuhama-hama, wao waweza kupatikana katika kila mkoa wa Visiwa Solomoni, baadhi yao hata wakiishi nje ya eneo lao la kikabila
kwa zaidi ya miaka 50. Basi haikuwa sadfa kwamba wakati Norman Sharein, kutoka tawi la Papua New Guinea, alipoenda kaskazini mwa Malaita katika 1962, yeye alipata mamia yao, wengi wao wakiwa na nia na hamu ya kukubali kweli ya Biblia.Wamalaita wengi walikuwa wamejihusisha katika harakati ya kisiasa iliyoshindwa ambayo ilijitahidi kupata uhuru kutoka kwa utawala wa Uingereza, iitwayo Ma’asina Ru’u (Ule Udugu). Wakihisi kuwa wamefarakishwa na makanisa madhubuti, waliunda dini yao wenyewe, Boboa (Msingi). Hata hivyo jina hilo, lilithibitika kuwa la kiunabii. Idadi kubwa yao ilikubali kweli ya Biblia na wakawa Mashahidi waliobatizwa ambao walifanya maendeleo na kuwa wahubiri hodari na mapainia. Wametumikia si kwenye idadi kubwa ya vijiji vya milimani vilivyo mbali katika eneo lao wenyewe la kikabila Malaita tu, bali kila mahali kotekote katika Visiwa Solomoni, bila kujali eneo ni la mbali na lililojitenga kadiri gani.
Habari Njema Zafika Mkoa wa Magharibi
Mojawapo Mashahidi wa kwanza kutumiwa katika kazi ya umishonari ya mahali hapo katika Mkoa wa Magharibi alikuwa Fanidua Kirite’e kutoka Malaita mashariki. Alikuwa mwanamume kijana mwenye familia huko nyuma katika 1967. Yeye na ndugu mwingine walijitolea kusafiri hadi Mkoa wa Magharibi
wakiwa mapainia wa pekee, wakielekeza jitihada zao kwanza katika Kisiwa Gizo.Wakati wa kukaa kwake kwa majuma mawili katika mji wa Gizo, Ndugu Fanidua alitiwa moyo aendelee kufanya kazi yake ya kuhubiri na msimamizi wa polisi katika wilaya hiyo, ambaye pia alimwambia yeye na mwenzi wake wawasiliane naye pindi wapatapo matatizo yoyote katika eneo lake la mamlaka, lililotia ndani kikundi cha visiwa New Georgia. Haukupita muda mrefu kabla ya mapainia kuwasili Munda, makazi ya watu katika wangwa wa Roviana kwenye Kisiwa New Georgia.
Munda hasa ni mkururo wa vijiji vidogo vilivyotawanyika kwenye mzingo wa uwanja wa ndege uliojengwa katika miaka ya mapema ya 1940 na Jeshi la Japan. Jeshi la Wanahewa la U.S. lilitwaa uwanja huo baadaye, likaupanua, na kuutumia muda wote uliobaki wa Vita ya Ulimwengu 2. Katika makabila yaliyoko eneo hilo, wanawake ndio huongoza familia. Ndugu Fanidua akumbuka hivi: “Tulipowasili Munda kwa meli ya serikali ya kupeleka barua, tulianza kujiuliza ni wapi tungekaa na ni nani
tungekaa naye na kweli ingepokelewaje katika eneo hilo geni. Tulitembea kwenye barabara ipakanayo na wangwa na upesi tukafika mbele ya nyumba ya Taude Kenaz, Mmalaita. Nilijua Taude angetukaribisha, kwa vile alikuwa Mkwara’ae mwenzangu, lakini kukaa kwetu katika makao yake tukiwa Munda, kulitegemea zaidi jinsi tungepokelewa na Miriam, mama-mkwe wake aliyekuwa mjane, aliyekuwa ndiye mwenye shamba.”Miriam alikuwa mshiriki maarufu na mwenye kustahiwa wa kabila la Roviana la Kisiwa New Georgia. Miriam hakuwa tu na uwezo akiwa mwenye shamba, bali alikuwa na uvutano mkubwa sana katika United Church. Mume wake aliyekuwa amekufa alikuwa amechangia sana katika kuingiza dini hiyo katika eneo lao. Kwa sababu Miriam alikuwa ameota mapema kuwa angepokea wageni fulani wasio wa kawaida, hakusadiki macho yake alipowaona mapainia wawili wakiwa na mikoba na Biblia mikononi, wamesimama mlangoni pake. Aliwakaribisha mara hiyo wakae katika nyumba yake, jambo lililowashangaza sana mapainia wale. Ukaribishaji-wageni wake ulithibitika kuwa baraka kwa familia yake nzima. Mapainia hao walikazia fikira kufanya mafunzo kila jioni na wote walioonyesha fadhili kama hiyo. Miriam na binti yake Esther na Taude, mume wa Esther, walikuwa watu watatu wa aina hiyo.
Ilikuwa katika kipindi hicho, katika 1970, kwamba waangalizi wasafirio John Cutforth na Jim Smith walipozuru Munda wakiwa njiani kurudi Papua New Guinea. Akitambua upesi uwezekano wa watu kupendezwa katika Munda, Ndugu Smith aliwaambia hao mapainia kuwa ingefaa wao wakae mpaka kutaniko lianzishwe. Hao waangalizi wawili walisaidia kwa bidii mapainia hao kupanga mikutano kitengenezo. Kwa mara ya kwanza, nyimbo za sifa kwa Yehova zingeweza kusikika katika kisiwa New Georgia! Wakiwaacha mapainia katika Munda kutunza kondoo, waangalizi hao wasafirio waliondoka kuelekea maeneo mengine.
Ghafula, jioni moja, wale mapainia waliamshwa kifedhuli na umati wa watu wenye kasirani. Genge hilo la watu liliongozwa na polisi mmoja aliyekuwa pumzikoni, ambaye aliwaamuru wale
ndugu watoke sehemu hiyo mara hiyo. Ndugu Fanidua akageukia umati na kuuambia yale ambayo msimamizi wa polisi alikuwa amewaambia katika Gizo: “Mpatapo matatizo yoyote katika eneo la mamlaka yangu, hakikisheni mnawasiliana nami.” Yule polisi aliposikia hivyo aliingiwa na wasiwasi, na umati nao ukafumukana. Hata hivyo, habari hiyo yenye udhia ilisambaa kwa kasi na kusikiwa katika Gizo na msimamizi mwenyewe.Msimamizi alipanda ndege mara hiyo kuelekea Munda. Upesi baada ya kuwasili, Ndugu Fanidua aliombwa afike kwenye kituo cha polisi cha mahali hapo. Alipoingia kituo hicho, Ndugu Fanidua aliona kuwa maofisa wawili wa vyeo vikubwa wa mahali hapo walikuwapo. Kisha akafahamu; mahojiano na msimamizi yalikuwa kwa faida ya wale maofisa wa polisi wawili wa mahali hapo. Baada ya Ndugu Fanidua kueleza kwa nini yeye na mwenzi wake walikuja Munda, msimamizi aliyajumlisha mazungumzo kwa kusema hivi: “Mimi ninayo dini, wewe, Albert, [akiashiria ofisa mmoja] unayo dini. Wewe, Alex, [yule mwingine] unayo dini yako. Sheria ya Visiwa Solomoni hulinda uhuru wa ibada kwa kila mtu. Mashahidi hao wanaishi kwa Miriam kwa mwaliko wake mwenyewe. Yeye ndiye mwenye shamba kidesturi, na anayo haki ya kisheria na ya kikabila kutembelewa na watu wa dini yoyote katika makao yake, na ninyi mkiwa maofisa wa sheria, mwe mko kazini au pumzikoni hamna haki ya kumzuia Miriam kuonyesha kupendezwa kwake kuwaelekea Mashahidi wa Yehova.” Alimalizia kwa kuwaweka mapainia hao wawili katika utunzi na himaya ya pekee ya maofisa hao wa polisi wa mahali hapo.
Ijapokuwa Ndugu Taude alikufa miaka kadhaa iliyopita, kutaniko dogo katika Munda laendelea kusitawi nalo husifu jina la Yehova kwa ukawaida kwa wimbo na kwa kazi ya kuhubiri. Na kwa habari ya Ndugu Fanidua, aendelea kuwa mpiga mbiu ya habari njema aliye mwaminifu.
Wamishonari Waruhusiwa Kukaa
Katika 1980, wamishonari waliozoezwa Gileadi walipewa viza ya kuingia Visiwa Solomoni. Wa kwanza kuwasili walikuwa
wenyeji wa New Zealand kutoka darasa la 67, Roger na Shona Allan. Hapo mbeleni, wamishonari na waangalizi wa mzunguko na wa wilaya kutoka tawi la Papua New Guinea walikuwa wakiruhusiwa kuingia kwa muda tu. Katika Aprili 1982, wamishonari zaidi walikuja, Arturo Villasin na Pepito Pagal kutoka Ufilipino. Msaada zaidi ulihitajiwa Ndugu na Dada Finlay walipoondoka kwenda Australia kwa sababu ya madaraka ya familia katika 1985. Katika mwaka uo huo, wamishonari wawili wenye ujuzi waliwasili, Josef Neuhardt wa darasa la 45 la Gileadi na mkewe, Herawati, waliokuwa wametumikia kwa miaka kumi katika Indonesia na miaka minane katika Papua New Guinea. Neuhardt aliwekwa kuwa mratibu wa Halmashauri ya Tawi. Kisha Loreto Dimasaka akawasili kutoka Ufilipino, na baadaye, Douglas Lovini wa darasa la 70 la Gileadi na mkewe, Luana, waliruhusiwa kuingia nchini, baada ya kutumikia miaka kadhaa katika eneo la Papua New Guinea. Yeye atumikia akiwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi.Msalaba Waangushwa Katika Mkoa wa Temotu
Karibu kilometa 900 kusini-mashariki mwa Honiara, kuna Mkoa wa Temotu, utiao ndani visiwa vya nje vya mashariki mwa Visiwa Solomoni, kutia ndani Visiwa Santa Cruz. Mkoa wa Temotu ulikuwa usio wa kawaida. Ni dini moja tu iliyowakilishwa huko, Kanisa la Anglikana. Kwa miaka mingi hakuna dini nyingine iliyokuwa imewavutia watu wa visiwa hivyo wenye kuchukua mambo kwa uzito. Lakini katika 1976, John Mealue, mhubiri asiyekuwa na cheo wa Anglikana, alipelekwa Papua New Guinea na kanisa lake kwa ajili ya mazoezi akiwa mtafsiri wa lugha za huko. Hali ya kidini ya mkoa huo ilikuwa karibu kubadilika.
Alipokuwa akiishi Papua New Guinea, asubuhi moja John alimfungulia mlango mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Yeye akapata mwonjo wake wa kwanza wa habari njema za Ufalme. Baada ya mazungumzo zaidi, John alitambua upesi kuwa yale aliyokuwa akisikia yalikuwa kweli ya Biblia. Ijapokuwa alikuwa amechaguliwa kuwa askofu wa Anglikana anayefuata wa Visiwa
Santa Cruz, yeye alijiuzulu kutoka kwa mafunzo yake ya lugha na kurudi Visiwa Solomoni. Akiwa njiani kuelekea Visiwa Santa Cruz, alipitia ofisi ya tawi katika Honiara na kuomba mtu azuru kisiwa chake kwa kusudi la kuanzisha kutaniko. Tawi likaanza mara hiyo kufanya mipango.Katika kijiji chake, John alianza kuhubiria ndugu zake wa kimwili, James Sopi na Drawman Alilvo, wote wawili wakiwa walimu, lakini walipinga ujumbe wake. Ndugu zake na watu wengine pia walitaka kujua kwa nini alirudi. Aliwajibu waziwazi na kuwaambia juu ya mtamauko wake kuelekea makasisi. “Wamekuwa wakitudanganya muda wote,” akasema, na akawapa mifano. Kumbuka kufikia wakati huo, John alikuwa hajapata kamwe kufunzwa jinsi ya kutoa ushahidi kwa busara. Pindi moja, akiwa na shoka mkononi, alikwenda hadi katikati ya kijiji cha Malo na kuukata msalaba wacho mkubwa, akaukokoteza chini, na kuutupa baharini. Hakuna mtu aliyedhubutu kumzuia. Hata hivyo, hakulazimika kutumia siku mahakamani tu bali kwa sababu alikuwa ameangusha mfano wao mtakatifu, viongozi wa kidini walibashiri kuwa John angekufa ghafula kabla ya siku nane kupita.
Siku nane baadaye John alikuwa bado yu hai. Hilo likatia alama wakati wa watu wa mfano wa kondoo kufanya badiliko kubwa. Habari juu ya hilo ilisambaa kama moto wa mwituni, na John alipofikishwa mahakamani, si kwamba tu jumba la mahakama la hapo lilijaa pomoni, bali Lata Station, jiji kuu la mkoa wa Temotu, lilikuwa limefurikwa na halaiki ya watu.
Kulikuwa na kimya kingi sana John alipoinuka kujitetea. Yeye alivuta dhamiri ya umati akiongea kwa kirefu juu ya asili ya msalaba, unafiki wa Jumuiya ya Wakristo, na jinsi makasisi walivyomweka yeye na watu wake, katika Enzi ya Giza, kiroho. Katika uamuzi wake, jaji alisema hivi: “Mashtaka yametupiliwa mbali. Hata hivyo, ni lazima ulipe faini ya dola 20 kwa kuharibu mali ya watu binafsi.”
Makasisi walishindwa; walikuwa wakitaka John ahukumiwe kifungo cha kazi ngumu gerezani. Watu kadhaa, wakiwamo
ndugu zake, James na Drawman, waliathiriwa na yale waliyosikia mahakamani na baadaye waliingia katika kweli.Njia ya Amani ya Kuhubiri
Katika 1981, Billy Kwalobili na Joe Kwasui waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Lata katika Mkoa wa Temotu wakiwa ndipo tu wametoka kwenye ujenzi wa tawi wa miaka miwili. Walitazamia kusaidia kusitawisha kweli katika eneo hilo jipya. Wahubiri waliostahili hivi karibuni walihitaji kujifunza kuwa “haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, . . . mvumilivu.” (2 Tim. 2:24) Kwa mfano, siku moja kikundi cha wahubiri kilipokuwa kikitoa ushahidi, genge la Waanglikana wenye kasirani, lililochochewa na makasisi, lilimshambulia mhubiri mmoja na kuamuru wengine wasihubiri katika kijiji chao. Wahubiri hao wapya walifikiri kuwa njia pekee ya kuhakikisha kazi ya kuhubiri inafanywa, ilikuwa kuondoa kizuizi kwa nguvu. Kwa hiyo walilipiga genge zima, wakavunja mguu wa mmojawapo wapinzani! Kwa furaha, kupitia kwa maagizo kutoka kwa Sosaiti na mfano wa mapainia, kukiwa na nyakati zenye wasiwasi, hatimaye wahubiri wapya hao walijifunza njia ya amani ya kuhubiri.
Billy na Joe walikabili matatizo mengine pia. Waangalizi wa mzunguko na wa wilaya walikuwa karibu kuwasili katika majuma matatu ili kufanya kusanyiko la mzunguko la kwanza katika Visiwa Santa Cruz. Hata hivyo, kulikuwa na shida moja kubwa; hakukuwa na mahali pa kufanyiwa kusanyiko. Jitihada za mara hiyo zilifanywa ili kupata mahali pa kujenga Jumba la Ufalme. Lakini mahali gani? Ingawa wengi waliopendezwa walikuwa wakiishi Nemba, kulikuwa na upinzani mkali kutoka kwa Kanisa la Anglikana. Kwa kusikitisha, wote wenye mashamba yaliyorithiwa walikuwa washiriki wa kanisa na walipinga kabisa kujengwa kwa Jumba la Ufalme katika ujirani wao. Kwa hiyo uamuzi ulifanywa kujenga katika kijiji cha nyumbani kwa John Mealue, katika kisiwa Malo, safari ya saa tatu kwa mtumbwi kutoka Nemba.
Mapainia walipomwendea John wakiwa na pendekezo hilo,
alijibu hivi: “Hivyo ndivyo hasa nimekuwa nikitaka kwa muda mrefu.” Kwa hiyo, siku iyo hiyo, ujenzi ulianza kwa kasi sana. Katikati ya ujenzi, mwangalizi wa mzunguko aliwasili kwa ziara yake ya kawaida kwa kutaniko, na yeye pia akajiunga nao katika kazi ya ujenzi. Kwa wakati barabara, jumba la majani lililojengwa vizuri, likiwa na paa, jukwaa, na pande tatu zilizokuwa wazi, lilikuwa tayari kukaliwa na umati uliotazamiwa kwa ajili ya programu ya kusanyiko.Baada ya muda John, James, na Drawman, pamoja na wake zao, walibatizwa. Ndugu hao watatu wa kimwili walithaminiwa sana na Kanisa la Anglikana, lakini baada ya wao kukubali kweli, makasisi waliweka msongo kwa wakuu wa elimu na kusababisha James na Drawman kufutwa kazi. Hilo halikuwazuia ndugu hao wawili. Waliamua kujiruzuku kwa kutegemea mazao ya ardhi na bahari na kutumia wakati wao kuhubiri nyumba kwa nyumba kuhusu hazina zilizo hazina kwelikweli, zile kweli nzuri ajabu za Ufalme. Upesi wengi zaidi walijiunga nao. Mwishowe Jumba la Ufalme lilijengwa katika Nemba. Kutaniko lilihamishwa baadaye kupelekwa katika kijiji cha Belamna.
Mapainia wa pekee Festus Funusui na mkewe, Ovature, walipewa mgawo kwenda Belamna katika 1988 ili kupanga zaidi kazi ya kuhubiri. Kutoa ushahidi barabarani na sokoni kulianzishwa jijini Lata Station. Hivi karibuni, katika kusanyiko la mzunguko, watu wapatao 200 walihudhuria. Ukuzi zaidi waweza kutarajiwa. Wanapanga kujenga Jumba la Kusanyiko lenye viti 500 katikati kabisa ya jiji la Lata Station. Bila shaka, Yehova amebariki ukuzi huo.
Umo “Tofauti” Katika Kisiwa Reef
Muda fulani baada ya John Mealue kukubali kweli, Michael Polesi wa Gawa katika Visiwa Reef, katika kikundi cha visiwa vya nje vya mashariki, alihudhuria Chuo cha Elimu ya Juu katika Honiara. Michael alikuwa Mwanglikana. Asubuhi moja, alipokuwa akitembea kupitia sokoni ambapo Mashahidi husimama chini ya mti watoapo ushahidi wa barabarani, aliona kwamba
wavulana wachanga walikuwa wakidhihaki baadhi ya wahubiri wazee-wazee. Mara nyingi mabezo yao yalimlenga hasa Benjamin Ru’u, Shahidi ambaye sehemu ya mguu wake mmoja ilikuwa imekatwa. Michael alipomwona akitembea kwa msaada wa mguu bandia uliounganishwa na kiungo cha goti lake, alimsikitikia Benjamin na kupata kutoka kwake kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele. Alikichukua alipokuwa akirudi Malo katika Visiwa Santa Cruz, ambako alikuwa akifunza katika shule ya msingi.Huko alifikiwa na Drawman nduguye John Mealue, ambaye bado alikuwa mwalimu wa shule ya msingi. Michael alifurahi kupata mtu wa kumsaidia kuielewa Biblia. Kwa kusikitisha, mwaka wa shule ulikaribia kumalizika, na Michael angerudi nyumbani kwenye familia yake katika Visiwa Reef. Kufikia wakati alipokuwa tayari kurudi nyumbani, alikuwa amesoma sura tatu tu za kitabu Kweli. Hata hivyo, ujapokuwa uelewevu huo mdogo wa Maandiko alianza kuhubiri nyumbani kwao.
Kwa sababu Michael hakuacha kusema peupe kuhusu kweli, makasisi waliwakaza wakuu wa elimu katika Lata Station wamfute kazi, sawa na walivyowafanya James na Drawman baadaye wafutwe. Michael aliamua kuitegemea ardhi kujiruzuku. Yeye na mkewe, Naomi, pamoja na watoto wao, walilazimishwa mwishowe kuondoka kijijini mwao wakiwa wamekataliwa. Wakiwa mbali na kijiji hicho, walijenga makao mapya na baadaye Jumba la Ufalme. Walipoondoka kijiji chao, waliondoka na kijibwa kiitwacho Tofauti, kwa kuwa kama Michael alivyoelezea, “Hii ni ishara kuonyesha kwamba hapana shaka sisi ni tofauti na ulimwengu.” Mpaka leo hii, kulingana na Michael, Tofauti ni kana kwamba ajua ile tofauti pia kwa maana “yeye huuma tu makalio ya wale wasiokuwa Mashahidi wa Yehova au wenye kupendezwa.”
Lakini turudie hadithi yetu. Baadaye, James Sopi, Billy Kwalobili, na Joe Kwasui waliwasili kwa meli kutoka Visiwa Santa Cruz kwa siku saba ili kumpa Michael kitia-moyo cha kiroho na kumsaidia atunze wanaopendezwa. Michael akawa
mhubiri mwenye bidii na baadaye akabatizwa kwenye mkusanyiko wa wilaya katika Honiara. Idadi ya wale waliojiunga na Michael kuwa wahubiri katika Visiwa Reef iliendelea kuongezeka. Kwa hiyo katika 1984, David Kirite’e na Ben Ramo waliwasili wakiwa mapainia wa pekee. Hata hivyo, mambo hayakuwa rahisi kwao.Majani Yapiga Kelele
Mojawapo matatizo iliyowapata David na Ben yalisababishwa kwa sehemu na uhasama uliopo kati ya wenyeji fulani wa Visiwa Reef na Wamalaita. Mtazamo huo wa chuki ulisitawi baada ya pigano kuzuka baina ya vikundi vya Anglikana vyenye ushindani katika Honiara karibu na wakati ambao mapainia hao waliwasili. Kwa hiyo ikawa vigumu kwa mapainia hao wa pekee Wamalaita kwenda mahali popote peke yao kuhubiri. Kuongezea shida yao, watu huishi wakiwa na hofu ya askofu na mapadre wao. Mara nyingi makasisi walikuwa wakiwatembelea watu kuona kama fasihi zozote za Sosaiti zingepatikana katika makao yao. Kama zozote zingepatikana, mwenye nyumba angepokea karipio kali na angelazimishwa kuitoa hiyo fasihi ili padre aweze kuiharibu. Hivyo, ikawa vigumu sana kumhubiria yeyote; watu walitoroka mara walipomwona Shahidi akija.
Mapainia waling’amua kuwa ingewabidi kutumia njia nyingine kuhubiri. “Tuliamua kutumia majani,” wakasema. “Tulikuwa tukienda mahali ambapo vijia vya vichakani hupitana na kuchuma jani kubwa la mti wa karibu na kuandika juu yalo andiko kwa herufi kubwa na, kwa herufi ndogo zaidi, tukaandika ufafanuzi wa andiko hilo. Kisha kwa herufi ndogo kwelikweli, tuliandika hivi: ‘Ikiwa wataka kuelewa mengi zaidi kuhusu andiko hili, tafadhali waandikie Mashahidi wa Yehova wa Visiwa Solomoni, au muulize Shahidi aliye karibu nawe.’”
David na Ben watuambia mfano mwingine wa utoaji wao wa ushahidi kwa kutumia majani: “Tulikuwa tukiandika kichwa ‘Ufalme wa Mungu,’ na kisha chini yacho, andiko la kwanza, Mathayo 24:14, na maneno ‘Lazima sisi tuhubiri juu ya huo.’ Na kisha swali chini yayo, ‘Huo Ufalme wa Mungu utafanya nini?’ Na kisha, andiko la mwisho, Ufunuo 21:4.”
Ikiwa hao mapainia walikuwa wakihubiri katika eneo ambapo watu walipinga sana kweli, wangetumia Zaburi 37:9 kama andiko la mwisho kwenye jani: “Maana watenda mabaya wataharibiwa, bali wamngojao BWANA ndio watakaoirithi nchi.” Kisha wangeacha jani hilo katikati ya vijia vya vichakani vilivyotumiwa sana na watu wengi zaidi na kwenda zao. Je! njia hiyo ya kuhubiri ilipata matokeo mazuri?
Siku moja mmojawapo mapainia aliandika mahubiri kwenye jani kwa kalamu ya wino na kuliweka kwa uangalifu katikati kabisa ya barabara iliyotumiwa sana. Alitembea mwendo mfupi na kujificha baina ya miti. Alingoja, akiwa na hamu kuona nani angelichukua jani hilo. Alishangaa kumwona mbwa akija huku akizurura-zurura na kutua ili kunusa lile jani. “Ninafikiri yule mbwa alijua kusoma,” alisema painia huyo kwa ucheshi, “kwa maana alianza kulibwekea jani. Mbwa alisisimka na kupiga kelele hivi kwamba mwindaji katika
kichaka kilichoko karibu alifikiri mbwa huyo alikuwa amemfanya posamu (aina ya mnyama kama komba) au mjusi anaswe juu ya mti. Mwindaji huyo alikimbia hadi mahali hapo akagundua tu kumbe mbwa alikuwa akibwekea na kukwaruza-kwaruza lile jani. Alimsukuma yule mbwa kando na kulichukua lile jani kwa uangalifu. Alitumia muda mchache kusoma mahubiri yaliyokuwa kwenye jani na kisha akaurudisha ujumbe wa jani katikati ya barabara kwa uangalifu uleule.”Yule painia amalizia hadithi hivi: “Baadaye nilipokuwa nikipita nyumba ya mwindaji huyo, aliniuliza, ‘Je uliweka kitu barabarani?’ Tulianza mazungumzo ya Kimaandiko ambayo upesi yalikuja kuwa funzo la Biblia la kawaida. Sasa mtu huyo na familia yake nzima ni wahubiri wa habari njema.”
Kipofu Aona
Billy Kwalobili alioa katika 1986, na yeye na mkewe Lina, wakapewa mgawo kwenye Visiwa Reef wakiwa mapainia wa pekee. Mojawapo wanafunzi wao wa Biblia waliyempenda sana alikuwa mwanamume kijana, aitwaye Eriki aliyekuwa kipofu. Eriki alipendezwa sana na milio ya ndege na wadudu na angeweza kuigiza milio hiyo kikamilifu. Kupitia funzo lake la Biblia pamoja na akina Kwalobili, alijifunza juu ya Yule aliyeumba viumbe hivyo vyote. Pia alijifunza kwa nini watu huugua na kwa nini yeye alikuwa kipofu. Billy angesoma kwa sauti mafungu yote ya funzo; Eriki angesikiliza kwa makini na kisha kujibu maswali ya mafungu hayo kwa maneno yake mwenyewe. Eriki alikariri akilini zaidi ya maandiko 30.
Mwangalizi asafiriye alipomzuru Eriki, yeye alipendekeza hivi: “Msimzuie. Acheni ahubiri.” Mwisho-juma huo Eriki alijiunga na wahubiri wanane walipokuwa wakitembea kupitia vichaka vilivyosongamana wakielekea kwenye eneo. Mwangalizi asafiriye alishika ncha moja ya mwavuli naye Eriki akashika ile nyingine, akifuata nyuma upesi. Pindi kwa pindi, angepaza sauti kusema: “Tahadhari! kuna gogo limekingama njia!” au “Chunga jiwe upande wa kushoto!” na kisha Eriki angeinua mguu na kutambuka lile gogo au apitie kando kuliepuka lile jiwe. Watu
wengi walimsikiliza Eriki akizungumzia tumaini lake, na alipoyanukuu maandiko kutoka akilini, walitikisa vichwa vyao kwa mshangao wakiandamana naye kwa kusoma Biblia zao.Mwishoni mwa ziara, Eriki alimwambia mwangalizi asafiriye hivi: “Kuna vitu vitatu ambavyo ningependa kuwa navyo kama ningekuwa na uwezo.” Alipoulizwa ni vitu gani hivyo, alijibu hivi: “Biblia, kitabu cha wimbo, na mkoba wa kutolea ushahidi!”
“Lakini kwa nini ungehitaji vitu hivyo, Eriki?” mwangalizi akauliza. Eriki akajibu hivi: “Ili niendapo kwenye Jumba la Ufalme au kuhubiri shambani, niwe kama ndugu na dada zangu. Niendapo kutoa ushahidi, huenda watu wasiamini nisemayo, lakini nikiwaonyesha maneno hayo katika Biblia yangu, wanaweza kuandamana nami kwa kusoma. Na ili niweze kuchukua Biblia yangu na kitabu cha wimbo, ninahitaji mkoba.” Upesi baadaye, Eriki alipewa zawadi mbili: Biblia mpya na kitabu cha wimbo. Kwa vile ndugu hawana mikoba ya ngozi, wao hukata mifuko ya mchele vipande viwili na kushona kanda za kupitisha begani juu yavyo. Eriki alipewa pia ‘mfuko wa mchele’ wake mwenyewe wa kutolea ushahidi. Ilikuwa kama ndoto inayotimia kwake. Kutaniko lote lilishiriki shangwe yake!
Upesi baadaye, Michael Polesi aliandikwa kazi tena kuwa mwalimu. Akiwa katika cheo hicho sasa angeweza kuwafikia watu wengi zaidi kwenye Visiwa Reef. Shangwe zaidi ilipatikana wakati wanawake wawili wa kwanza kutoka Visiwa Reef walipobatizwa katika 1990 kwenye kusanyiko la mzunguko katika Visiwa Santa Cruz. Hapana shaka, kuna mambo mengi mazuri katika wakati ujao kwa ajili ya Mkoa wa Temotu.
Habari Njema Zafika Mkoa wa Makira
Katika 1984 eneo lililokuwa bado kutembelewa na Mashahidi wowote lilifunguka. Kilikuwa kisiwa San Cristobal, ambako maeneo ya vijiji vya kikabila yalikuwa bado na udhibiti mkubwa. Ilikuwa vigumu kuwapa mapainia mgawo kwenye kisiwa hicho kwa sababu njia ya maisha ya kikabila haikuruhusu wageni. Hata hivyo, mambo yalionekana maangavu zaidi wakati ndugu
aliyekuwa mwendesha mashine ya vyombo vizito alipopelekwa San Cristobal na kampuni yake. Upesi tawi lilitumia fursa hiyo kwa faida na kumtuma James Ronomaelana, painia wa pekee na ambaye sasa ni mshiriki wa Halmashauri ya Tawi, kwenda San Cristobal kuchanganua uwezekano wa kuanzisha kazi.Alipokuwa akitoa ushahidi kisiwani, James alistahimili upinzani mwingi mwanzoni, na siku moja alishangazwa kupata ilani iliyokuwa na onyo lenye kusema: “Watu wa Yehova! Msiingie bila ruhusa ya kuingia.” Hata hivyo, pindi nyingi kama hizo za kuvunja moyo hazikupoza bidii yake, ambayo kwayo alibarikiwa kuona mambo mengi ya kusisimua. Asimulia hivi: “Katika kijiji kimoja, nilifika kwenye nyumba kubwa. Mwanamume mwenye nyumba alimiliki shamba kubwa la minazi na ng’ombe na hapana shaka alikuwa tajiri zaidi ya majirani wake. Kwa hiyo, niliepuka nyumba hiyo nikifikiri kuwa mwanamume huyo hangekuwa na wakati kwa ajili ya kweli. Nilipokuwa nikienda zangu, nilianza kuhukumu vitendo vyangu vya woga. Nilijiuliza kwa ukali, ‘Kwa nini ninaepuka mahali hapa?’ na kisha nikajijibu kijasiri, ‘Yehova amenituma hapa, na pengine hii ndiyo mara yangu ya mwisho kuwa hapa. Ni sharti niende na kusema na mwanamume huyo!’”
Alipofika nyumba hiyo, alikutana na wenyewe, Oswald na Rachel Oli. James alianzisha mazungumzo kwa shauku kwa kuonyesha kwamba Mungu analo jina, na yeye ana kusudi kwa dunia. Mume na mke hao walifurahi kujifunza kwamba Mungu atarudisha tena dunia kuwa paradiso. Kwenye ziara ya pili, funzo la Biblia lilianzishwa. Oswald na Rachel walianza upesi kupatanisha maisha zao na kanuni za uadilifu za Yehova. Kwa vile Oswald alikuwa akitoa mchango mkubwa kwa kanisa, haikuwa ajabu wakati upinzani mkali kutoka kwa Kanisa la Anglikana ulipoletwa dhidi yake. Wakati uo huo, mapainia wa pekee walipewa mgawo wafungue zaidi eneo hilo, jambo lililozidisha sana kasirani ya mapasta wa mahali hapo, hivi kwamba hata waliwaagiza washiriki wao kutumia jeuri ili kunyamazisha mapainia hao.
Wala mapainia wala hao Oswald na familia yake hawakuzuiwa. Kwa mfano, wakati Hankton Salatalau, painia wa pekee, alipokuwa akitoa ushahidi kwa mtu aliyependezwa, mshiriki wa Kanisa la Anglikana alianza kumtukana Hankton kwa sauti kubwa. Hankton alipoondoka kwa staha, mwanamume huyo alimshambulia kikatili kutoka nyuma na kumbwaga chini kwenye miamba ya matumbawe yenye ncha kali, huku akimpiga mateke mwilini bila huruma kwa zaidi ya dakika 15. Watu wa kijiji walipigwa butaa huku wakitazama kwa hofu kuu. Hata hivyo, hofu yao kuu kuelekea mapasta wao iliwazuia wasimsaidie. Hankton alilala chini bila msaada akikinga kichwa na mwili wake kwa mikono yake. Mgongo wake uliojaa damu ulionekana kama kipande cha nyama mbichi kwa kukatwa-katwa na miamba. Hatimaye, baadhi ya wanakijiji walipata ujasiri na wakaingilia kuamua. Walimshika mshambulizi na kumzuia, naye Hankton, aliyekuwa amepigwa kwelikweli, akaenda nyumbani.
Inasikitisha kwamba wenyeji wengi wa kisiwani bado wamenaswa katika utandobui wa hofu ya kanisa. Hata hivyo, baadhi yao wameanza kuona tofauti kati ya Ukristo wa kweli na Jumuiya ya Wakristo. Wakati uo huo ustahimilivu wa hao mapainia wa pekee wanne umethawabishwa. Makutaniko mawili yenye bidii, na yenye furaha yasitawi katika San Cristobal. Oswald, Rachel, na watoto wao, pamoja na familia ya Rachel, sasa ni wahubiri wasio na hofu wa habari njema pia.
Desturi Zisizo za Kawaida
Katika sehemu nyingi zisizofikika za Malaita, hasa milimani, pamoja na katika vile visiwa vingine, kuna makabila ambayo yanajua machache sana juu ya ama Jumuiya ya Wakristo au Ukristo wa kweli. Kimsingi wao huabudu wazazi wa kale, lakini baadhi yao ni waabudu wa viumbe.
Elson Site, aliyekuwa mwangalizi wa mzunguko na ambaye sasa ni painia wa pekee akiwa na familia ya watoto wanane, aelezea jinsi hali zilivyo katika baadhi ya maeneo hayo: “Ni desturi katika makabila watu kuvaa nguo chache au kutokuvaa chochote kabisa, na yeyote aliyevaa nguo atembeleapo kijiji
kama hicho, hutiliwa shaka na mara nyingi huzuiwa kuingia kijijini.”Wangeshughulikiaje hali hiyo ngumu? Elson aendelea hivi: “Pindi moja kikundi kutoka kutaniko dogo kiliwasili kijijini humo ili kuhubiri, na chifu akapinga ama ndugu ama dada kuvaa nguo wakiwa kijijini. Ndugu walieleza kuwa haikuwa desturi ya Kikristo kutembea uchi. Kwa vile walikuwa wamesafiri mwendo huo wote kuja kushiriki habari ya maana kutoka Neno la Mungu, wangetaka sana kutatua tatizo hilo dogo lililokuwa likizuia watu wake wasisikie habari njema hizo. Chifu alishauriana na wazee wa kijiji kwa kipindi kirefu sana na hatimaye akaamua kuwa haingewezekana kwa ndugu kuhubiria wanakijiji siku hiyo. Lakini mipango ilifanywa ili kufanikisha zaidi ziara wakati ujao. Wanakijiji waliahidi kujenga nyumba ya majani nje kidogo ya mpaka wa kijiji ili ndugu na dada, wakiwa wamevaa nguo kikamili, waweze kutumia nyumba hiyo kukutana na yeyote wa wanakijiji aliyetaka kuja katika nyumba hiyo kusikia yale ambayo Biblia hufundisha. Jambo hilo lilifaulu vizuri, kwa vile wanakijiji hufurahia kuzungumza mambo ya kiroho.”
Zaidi ya kulazimika kustahi vizuizi vinavyohusu nguo katika baadhi ya vijiji, sharti ndugu wafuate vizuizi vingine vinavyotumiwa na watu hao kutokana na itikadi zao. Arturo Villasin, ambaye sasa ni mwangalizi wa mzunguko, aripoti hivi: “Ndugu waongozao kikundi chochote cha kutoa ushahidi huwa waangalifu sana kustahi jambo la kwamba wanakijiji huwa na hisia zenye nguvu sana kuhusu kufanya chochote kitakachoudhi roho. Katika baadhi ya vijiji, kutaja maneno au majina fulani kulipigwa marufuku, kama vile kusema jina la kibinafsi la mzazi wa zamani mfu anayeaminiwa kuwa na uwezo juu ya kijiji. Baadhi ya miti pia huonwa kuwa mitakatifu, na ni wanaume peke yao wawezao kukaa chini ya vivuli vyayo. Katika kijiji kimoja hususa kilichoko karibu na bahari, kuvaa nguo za rangi fulani kunaudhi; nguo nyekundu na nyeusi haziwezi kuvaliwa. Kwa hiyo, kwa kutumia busara, kitabu au
Biblia yenye jalada jekundu au jeusi haitatumiwa ushahidi unapotolewa.“Kuna sehemu nyingine kijijini ambazo ni marufuku mwanamke kuingia. Mwanamume hawezi kukalia kiti kimoja na mwanamke asiye mkewe. Ikiwa mojawapo ya desturi hizo inakiukwa, sharti fidia ilipwe mara hiyo. Kwa hivyo ni muhimu kwamba ndugu na dada wawe na maarifa mengi juu ya kanuni, sheria na vizuizi vya kila kijiji hususa iwapo kutoa ushahidi kutafanikiwa. Hivyo, kabla ya kuingia kijijini, ndugu anayeongoza atazungumza kirefu kile hasa wale walioko kikundini watafanya au hawatafanya kijijini, hususa akina dada, ambao wanaelekea kukiuka pasipo kujua desturi zinazohusu wanaume. Marekebisho yasiyovunja kanuni za uadilifu za Yehova hufanywa kwa utayari ili wanakijiji wapate fursa nzuri ya kusikia habari njema. Wanakijiji wengi wameitikia na wameacha kwa shangwe mazoea yasiyompendeza Mungu wa kweli.”
Chazungukwa na Mashetani
Katika wilaya yenye milima-milima ya Kwaio katika Malaita kuna kijiji cha Aiolo. Familia za Mashahidi wa Yehova ndio wengi katika kijiji hicho.
Aiolo ni kama kimbilio kwa watu wa Yehova, kikiwa kimezungukwa na ibada ya mashetani. Utazamapo nje ya kijiji, waona maeneo mengi yaliyo mashamba matakatifu, vichaka vilivyosongamana kwenye vilele vya vilima, huku pande za vilima zikiwa zimelengetwa ili kutofautisha mashamba matakatifu na eneo jumuiya. Kuhani hutoa dhabihu ya nguruwe kwa miungu huko. Sehemu ya dhabihu huliwa na kuhani na wakati mwingine, na wanaume wengine. Hata hivyo, hakuna mwanamke anayeruhusiwa kula yoyote ya dhabihu hizo wala kushiriki katika kutoa dhabihu au sivyo atapata adhabu ya kifo, ingawa wanao wajibu mkubwa katika kufuga nguruwe. Baada ya kutoa dhabihu, makuhani au wengine watoao dhabihu sharti wabaki katika nyumba takatifu ndani ya mipaka ya kijiji kwa hesabu ya siku zilizowekwa kabla ya kuzirudia familia zao.
Nyumba ‘iliyojengwa upesi’ iliyotengenezwa kwa mianzi na vifaa vingine vya vichakani, ilijengwa Aiolo. Shahidi mmoja aliandaa nyumba hiyo mpya kwa ajili ya wale walioitwa eti watoro. Hao walikuwa watu wanaopendezwa, hata familia, zilizokimbia kutoka ibada ya mashetani. Wamekimbia vijiji vyao vinavyoabudu mashetani kutafuta kimbilio katika Aiolo. Wakati mmoja, familia ya watoro, mume, mkewe, na baadhi ya ndugu na dada zake, waliwasili kwa sababu wanakijiji walitaka kuwaua kwa ajili ya kumuudhi shetani wao kwa kutokutoa dhabihu ya nguruwe kwake. Adhabu—kifo!
Siku kadhaa baadaye mwangalizi asafiriye alizuru Aiolo. Sikiliza yale aliyo nayo ya kusema: “Mke wangu na mimi, tulialikwa kwa mlo katika kao la ndugu mmoja. Ile familia ya watoro ilikaa katikati yao. Tuliwapenda mara hiyo, lakini walikuwa na woga nao walituelekeza migongo yao. Hata hivyo, kufikia wakati ambapo mlo ulimalizika, walikuwa wakitabasamu sana na waliketi wakituangalia ana kwa ana. Walikuwa wametambua kuwa tulikuwa sawa tu na ndugu na dada wengine wote wampendao Yehova na ambao hupendwa na yeye pia!”
Hakuna Suruali Ndefu
Lakini acha turudi kwa Ndugu Villasin na kumuuliza kwa nini sasa yeye huvaa suruali fupi badala ya ndefu. Yeye asema
hivi: “Katika kijiji kimoja kikundi chetu cha wahubiri kilikuwa kimetoa ushahidi kwa kila mtu kijijini. Hata hivyo, ndugu mmoja alikuwa akizungumza kirefu na chifu wa kijiji. Hatimaye, ndugu yule alitoka ndani ya nyumba ya chifu. Uso wake ulikuwa na wasiwasi. Chifu alimwambia kuwa alitaka suruali yangu ndefu! Sasa nikawa na wasiwasi! Sikuwa na suruali ya ziada, na haikufaa kwa mwangalizi wa mzunguko kutembea bila suruali. Nilimwomba ndugu arudi upesi na kumsadikisha chifu kuwa ingawa yeye na watu wake waliona kuwa sawa kabisa kwenda uchi, mimi nilikuwa mtu wa kutoka nchi tofauti yenye desturi tofauti kabisa, na mojawapo ilikuwa kutokuonekana uchi hadharani kwa vyovyote vile. Lakini chifu alitamani suruali yangu ndefu. Hata hivyo, baada ya mazungumzo marefu, ndugu yule alimsadikisha chifu aniachie suruali yangu ndefu. Nilifarijika wee! Tokea wakati huo, sijavaa surali ndefu niendapo katika kijiji chochote. Mimi huvaa suruali fupi kama wale ndugu zangu wengine!”Mwangalizi asafiriye mwingine mgeni alipata ono la kutisha. Katika kijiji kimoja, mtu hapaswi kutumia maneno ya Kiingereza yaliyopigwa marufuku “wicked” (uovu) na “war” (vita). Maneno hayo mawili ni majina ya mashetani wao wawili. Kuyataja majina hayo ni hatia na fidia kubwa sharti ilipwe na mwenye hatia. Mashahidi wa mahali hapo walipokwenda kuhubiri huko, mwangalizi asafiriye mpya aliwaambia ndugu kuwa ingekuwa bora yeye asikilize tu kwenye kila mlango. Ndugu hawakukubali; walisisitiza kuwa mwangalizi asafiriye aseme mlangoni, kwa vile alikuwa amefundishwa vizuri desturi za mahali hapo. Ndugu aliyekuwa akizuru alikubali hatimaye. Alipokuwa akipanda na kushuka milima kwenye kijia cha vichakani, alikuwa akijiambia kwa sauti ya chini hivi: “Usiseme WAR, usiseme WICKED.”
Walipofika mwishowe kwenye eneo, mwanamume mmoja alimkaribisha mwangalizi asafiriye na ndugu wengine wawili katika nyumba yake. Ndugu hao wawili walianzisha mazungumzo na kisha wakasema mazungumzo yangeendelezwa na mwangalizi asafiriye aliyekuwa na wasiwasi. Alifanya utoaji mfupi wa kimaandiko, na mambo yote yakaenda vizuri. Mwenye nyumba
alionekana amefurahishwa na yale aliyoyasikia. Mwangalizi asafiriye alifurahi pia na kufungua kitabu Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani naye akaanza kuonyesha picha juu ya paradiso. Lakini ndipo, kwa hofu kuu yake, akaongeza hivi: “Na Mungu atafutilia mbali war [vita].”Yule mwanamume alikodoa macho yake, na ndivyo na mwangalizi asafiriye. Aliwatazama upesi ndugu hao wawili apate msaada naye akapumua kwa nguvu, lakini wao walimtazama mwenye nyumba kana kwamba wanasema: “Hakusema ‘war’ [vita], sivyo?” Mwenye nyumba naye aliwatazama kana kwamba anasema: “La, ninadhani hakusema hivyo.” Na hivyo mazungumzo yakaisha bila kuwa na lazima ya kulipa fidia yoyote. Lakini kwa habari ya mwangalizi asafiriye, alitamani sana kurudi Aiolo.
Si kwamba tu desturi na mitindo ya mavazi ya watu wa Solomoni ni tofauti na ile ya Magharibi bali pia njia za ujenzi hutofautiana. Hata hivyo, miradi miwili mikubwa ya ujenzi imewasaidia watu wengi wa huko kuona kwamba roho ya Yehova Mungu iko juu ya waabudu wake. Katika 1989 watu wa Auki katika Malaita walishangaa kuona kutaniko la wahubiri 60 likijenga Jumba la Kusanyiko ambalo wahudhuriaji zaidi ya elfu moja waweza kuketi ndani. Kisha, katika Juni 1991, watu wa Honiara walikodolea macho Jumba la Kusanyiko lenye viti 1,200 lililoonekana kana kwamba latokea ghafula katika misingi yalo kwa majuma mawili tu, jumba la kwanza la ukubwa kama huo kujengwa upesi katika sehemu ya Pasifiki. Kituo cha kwanza katika ziara yetu kwenye mahali pa ujenzi ni kisiwa Malaita.
“Jumba Alilojenga Yehova”
Anza na nyundo mbili na patasi mbili vikiwa vyombo. Ongeza wafanyakazi kadhaa wenye nia na mbao zote unazoweza kukata kutoka kwenye msitu wenye matope-matope ulio karibu. Sasa una vifaa vya kutosha vya kujenga Jumba la Kusanyiko lenye viti 1,500 kwa mtindo wa Visiwa Solomoni. Muujiza kama huo wa ujenzi umechochea sauti kuu ya kulisifu jina la Yehova katika Malaita. Ilibidi kutatua matatizo mengi mno yaliyoonekana kana kwamba hayatatuliki katika ujenzi wa kifaa hiki chenye
meta 930 za mraba hivi kwamba kilikuja kujulikana kuwa “jumba alilojenga Yehova.”Katika Juni 1982 wamishonari waliopewa mgawo katika Malaita walifanya mkutano katika Auki, mji mkuu mkoani, wakafikia mkataa huu: Jumba la Ufalme jipya kwa ajili ya kutaniko la mahali hapo la wahubiri 65 lilihitajiwa haraka. Roger Allan na wamishonari wawili Wafilipino, Pepito Pagal na Arturo Villasin walikuwa katika mkutano huo.
Jumba la Ufalme la kale lilikuwa limeshambuliwa na mchwa. Lilikuwa limelegea sana hivi kwamba upepo kidogo tu ulitisha kuliangusha. Likiwa limejengwa mwanzoni kuandaa kinga kwa kitambo dhidi ya jua na mvua kwa watu 400 waliokuwa wamehudhuria mkusanyiko katika Auki miaka 15 iliyokuwa imepita, lilikuwa sasa katika siku zalo za mwisho.
Kutaniko la Auki lilikuwa na ndugu wawili tu walioajiriwa kazi kikamili, na mshahara wao ulikuwa karibu dola 50 za U.S. kwa mwezi kila mmoja. Kwa hiyo washiriki wote wa kutaniko walikubali kukaza fikira kwanza juu ya kupata pesa za kuanza mradi huo. Ndugu Pagal na Villasin walipewa mgawo wa kupanga “chama” cha kutaniko—kikundi cha waliojitolea kutoka kutanikoni kufanya kazi ili kupata pesa zilizohitajiwa.
Kutaniko likakuza mimea yalo lenyewe ya viazi vitamu na kabeji. Kisha mazao yalipakiwa kwenye vikapu vilivyofumwa kwa majani ya mnazi na kupelekwa kwa meli hadi Honiara. Huko, ndugu mmoja painia mzee-mzee, Cleopass Laubina, aliuza mboga hizo kwa bei nzuri zaidi kadiri alivyoweza kupata na kupeleka pesa kwa kutaniko katika Auki. Pia, siku za Jumatatu, kati ya ndugu na dada 40 hadi 50 walifanya kazi ngumu ya kutosha jasho ili kuchuma pesa, kwa kuchimba mitaro, kuondoa magugu katika mashamba ya minazi, na kuchanganya saruji kwa mikono. Hivyo, kufikia 1985, baada ya kufanya kazi kwa miaka 3 1⁄2, kutaniko lilikuwa limekusanya hazina ya ujenzi ya dola 2,000 za U.S.
Panueni Mradi
Wakati uo huo, iliamuliwa kupanua sana mradi wa ujenzi kwa lengo la kunufaisha makutaniko yote 23 katika Malaita. “Badala ya kujenga Jumba la Ufalme kwa ajili ya wahubiri wapatao 70, kwa nini tusijenge Jumba la Kusanyiko kwa ajili ya watu wapatao 1,500?” Mashahidi wa huko wakasababu. Kwa hiyo ujenzi wa jengo kubwa ulipangwa ambao watu 1,500 wangeweza kutoshea na ambalo lingeweza kutoa kinga si dhidi ya jua kali la ikweta tu, bali pia dhidi ya mvua kubwa ya mara kwa mara iliyo kawaida katika Visiwa Solomoni.
Plani iliyochorwa vivi-hivi ilionyesha jumba lenye urefu wa meta 30 na upana wa meta 32, likiwa na paa yenye mwinamo kuelekea juu ili kuruhusu hewa yenye joto ipaayo itokee upande wa chini wa dari. Jumba lilinuiwa kujengwa bila mihimili katikati ili hadhira isizuiwe kuona mbele. Lingejengwa kwenye uwanja wa kutaniko wa ekari tano.
Katika 1985 halmashauri ya ujenzi ya kutaniko ilipokea mkopo wenye kutozwa riba ndogo. Muda mfupi baadaye, Mashahidi katika Swedeni walitoa mchango mkubwa, hivyo wakiipa hazina ya Jumba la Kusanyiko jumla ya dola 13,500 za U.S. ili kuanzisha kazi ya ujenzi.
Meneja wa kinu cha kupasua mbao katika Honiara pia aliahidi kutoa ugavi wa magogo yote 300 yaliyopasuliwa yaliyohitajiwa kwa ajili ya nguzo kuu za utegemezo na mihimili ya varanda na ya ukumbi pamoja na mikingiko ya paa ikiwa na fito na makombamoyo. Mikingiko ingeunganishwa Honiara na kisha kubomolewa na kusafirishwa kwa mashua hadi Auki, ambapo ingeunganishwa tena na kujengwa juu ya nguzo kuu za utegemezo.
Kikundi cha wafanyakazi wa ujenzi kilikuwa na hamu na utayari wa kuanza! Hata hivyo, vyombo pekee walivyokuwa navyo ni nyundo mbili na patasi mbili. Hapana shaka, kulikuwa na wasaidizi wengi wenye nia waliokuwa tayari kutoa msaada kazini. Lakini hakuna Shahidi katika Honiara aliyekuwa na ujuzi wowote wa ujenzi wa kibiashara. “Ndugu na dada walinitarajia
nitoe uangalizi katika kazi ya ujenzi, lakini nilikuwa sijawahi kujenga hata kibanda cha kuku!” akasema Ndugu Allan.Mashahidi hao wangewezaje kunyanyua toka chini mikingiko ya paa—kila mmoja ukiwa na magogo manane makubwa yaliyokongomelewa pamoja na yenye uzani wa kutoka tani mbili hadi tano—mpaka juu ya nguzo za utegemezo zenye urefu wa meta 6? Na, isitoshe, wangewezaje kunyanyua kilele cha paa meta 12 hewani bila kutumia mitambo ya kuinulia vitu vizito ujenzini?
“Sijui,” akaungama Ndugu Allan wakati ule. “Itabidi tu tumtegemee Yehova atusaidie.”
Msaada Wakaribishwa
Msaada wenye ustadi ulikuja kutoka ng’ambo ya bahari katika Oktoba 1986. Jon na Margaret Clarke, waliokuwa wameshiriki katika ujenzi wa ofisi ya tawi ya New Zealand, walisikia juu ya tatizo la Kutaniko la Auki nao wakaweza kupata viza ya kuzuru Malaita kwa miezi mitatu.
Likiwa limepewa kichanganya-saruji kuwa zawadi, kutaniko lilijenga jukwaa kubwa na ukuta wa saruji wenye vyumba pembeni nyuma ya jukwaa. Wakitumia mikono mitupu kuwa kolego, walichimba mashimo yenye vina na kuyajaza saruji, na kutia ndani nguzo kuu 18 za utegemezo kwa ajili ya ukuta, paa na varanda.
Baada ya kupokea mazoezi kutoka kwa Ndugu Clarke, ndugu wa huko wenyewe waliunganisha mikingiko ya paa la jumba kuu na mikingiko mitatu ya paa ya ukumbini. Lakini bado walikuwa na tatizo la kuweka mikingiko hiyo mahali payo. Lilikuwa tendo la ajabu kiuhandisi, kwa sababu mikingiko hiyo ilitengenezwa kwa kuyakongomelea magogo manane pamoja katika pembe tatu kubwa. Kupiga moyo konde na mbinu za ndugu hao ni vigumu kueleza.
Dansi ya Magogo
Vyombo pekee kwa ajili ya kazi ngumu ya kuinua vilikuwa kipande cha gogo na kamba zilizokuwa kwenye kreni ya kutumiwa
kwa muda. Kreni yenyewe ilikuwa imetengenezwa kwa magogo manane. Mkingiko wa kwanza, wenye uzani wa tani mbili, ungeinuliwa juu ya ukuta mpya wa saruji na kuwekelewa juu ya nguzo mbili za utegemezo zilizokuwa nyuma yao. Kreni ilipoinua wima mkingiko kwa kukamata kilele chao, ndugu walifadhaika kwa kung’amua kwamba, kreni hiyo haingeweza kuinua mkingiko juu vya kutosha kupitia ukuta. Urefu wa kreni ulipungua kwa meta moja! Kwa siku mbili mkingiko uliachwa ukining’inia kwenye kreni—ukiwa umeegemezwa kwa magogo upande wa chini—huku ndugu wakiomboleza na kuwaza juu ya tatizo hilo.Watu walikuwa wakipita na kuwadhihaki, wakisema hivi: “Yehova hawezi kuwainulia mkingiko?”
“Vema!” Ndugu walisema kwa dhati. “Sasa Yehova atatusaidia kwa hakika!”
Ubunifu wa ghafula uliwachochea wafanyakazi. Jeki kutoka kwa lori moja ya pick-up ilisukumwa chini ya ncha moja ya mkingiko na kuuinua sentimeta kadhaa juu. Kisha ncha hiyo ya mkingiko ilitegemezwa. Kisha jeki ilipelekwa kwenye ncha nyingine ya mkingiko ili kuiinua ncha hiyo, nayo pia ikainuliwa na kuegemezwa. Hatua hizo zilirudiwa tena na tena mpaka, baada ya siku nne za kuinua-inua, mkingiko wa kwanza ulikuwa umeinuliwa juu ya ukuta wa saruji na kuwekwa kwenye nguzo za utegemezo zilizokusudiwa. Mafanikio hayo makubwa yalifanya ndugu wacheze dansi kwa kuzunguka eneo la ujenzi kwa kufanya duara kubwa, wakipiga makofi na kuimba nyimbo za furaha.
Ilikuwa tu baada ya mradi kumalizika na jeki kuwa imetumiwa kuinua mikingiko mitatu—mmoja ukiwa na uzani wa tani tano—ndiposa ndugu wakang’amua kwamba maneno yaliyofutika-futika yaliyopigwa muhuri kwenye upande mmoja wa ndani wa jeki yaonyeshayo uwezo wayo wa kuinua hayakuwa “tani 15,” kama walivyokuwa wakifikiri, bali kwa hakika, yalikuwa “tani 1.5” tu!
“Nifikiriapo, yale ambayo ndugu na dada hao walifanya yanashinda akili kuelewa,” asema Ndugu Allan. “Kutazama
mikingiko hiyo mikubwa ikipanda hewani ilikuwa sawasawa na kutazama dansi ya magogo!”“Je! Yehova Hawezi Kujenga Jumba?”
Katika Januari 1987 ndugu wawili wazaliwa nchini waliokuwa na stadi katika ujenzi walizuru Auki kutoka Honiara na baada ya kukagua mikingiko walisema kwamba wenye kinu cha kupasua mbao walisafirisha bila kujua magogo ya mitunda isiyofaa na kwamba magogo hayo yalikuwa yakielekea kuoza bila kujulikana kutoka ndani na kuelekea nje. Waliamini sehemu ya katikati ilikuwa imeanza kuoza na kwamba ingebidi kubadilisha magogo yote. Miezi minne baadaye ugunduzi huo wa kuhuzunisha ulithibitika kuwa kweli—magogo mengi yaliyokuwa yameletwa yalikuwa yakioza, na ilibidi kurudia tena sehemu kubwa zaidi ya kazi nzito ya ujenzi iliyokuwa imekamilishwa.
Ndugu na Dada Clarke walirudi tena Auki katika Julai, wakiandamana na Steven na Allan Brown wa Auckland. Walikuja na vifaa vilivyotolewa kuwa upaji kutoka mahali pa ujenzi wa tawi la New Zealand lililokamilishwa. Ndugu hao kutoka New Zealand walipanga ziara yao wakiwa na lengo la kumalizia ujenzi wa paa la Jumba, lakini badala yake, kazi yao ilikuwa sasa kubomoa sehemu kubwa ya ujenzi wa mwaka uliotangulia.
Hata hivyo, tatizo kubwa zaidi walilokabili ndugu hao ni masuto ya daima kutoka kwa abiria waliokuwa wakipita kasi karibu na mahali pa ujenzi wakiwa ndani ya vilori vilivyo wazi nyuma, pamoja na maneno yenye kushusha heshima yaliyosemwa na watu sokoni na barabarani katika Auki.
“Je! Yehova hawezi kujenga jumba?” walifanya mzaha. “Hilo lathibitisha mnaabudu dini bandia,” walidhihaki. “Ni watu wenye kichaa tu ndio wawezao kujenga jumba kisha kulibomoa tena.” Watu wa dini nyingine walipopita karibu na mahali pa ujenzi, walicheza dansi na kuimba mbele ya wafanyakazi wenye kuhuzunika—wakishangilia kwa ajili ya msiba wao. Ndugu wenyeji walivunjika moyo sana hivi kwamba waliwaambia wale wamishonari wanne kwamba “tungeenda zetu mbali na jumba hili sasa hivi kama jina la Yehova lisingekuwa juu yalo.”
Dhihaka ya Kitambo Tu
Dhihaka ya wadhihaki mara nyingine ilikuwa ya kitambo tu. Kwa mfano, kikundi cha waimbaji wa nyimbo za krismasi kilikuwa kikielekea kwenye shughuli za pekee za kanisa umbali wa kilometa 16 kilipopita kwa kilori kiliwatukana na kuwacheka wafanyakazi wa ujenzi. Kilometa moja tu kutoka kwenye mahali pa ujenzi, lori yao iliharibika, wakiwa wamekwama, hawakuweza kufika walikokusudia kwenda.
Habari za kuharibikiwa lori yao zilipofika mahali pa ujenzi, shauri lilitolewa dhidi ya kulipa mtu “ovu kwa ovu.” (Rum. 12:17) Lakini baadaye kidogo wakati baadhi ya ndugu waliochukuliwa nyuma ya lori ya ujenzi walipowapita waimbaji wa nyimbo za krismasi waliokwama, hawakuweza kujizuia kucheza dansi kidogo kuonyesha shangwe yao!
Kijiji cha Kona Chasaidia
Ni magogo 38 tu kutoka kwenye kinu cha kupasua mbao yaliyokuwa hayajaanza kuoza, kwa hiyo baki la magogo 300 yaliyohitajiwa ilibidi yatolewe mahali pengine. Lakini yatoke wapi? Mashahidi kutoka kijiji cha Kona, kilichokuwa kilometa tano kutoka mahali pa ujenzi, waliwaendea wafanyakazi wa ujenzi ili watoe upaji wa miti ya pekee yenye mbao ngumu kutoka katika mashamba yao wenyewe. Mbao hizo zingechukua mahali pa nguzo kuu za utegemezo, mihimili ya varanda na ya ukumbini, na mikingiko ya jumba kuu. Hiyo ilikuwa dhabihu kubwa iliyotolewa na Mashahidi hao kutoka kijiji cha Kona, kwa vile Malaita kilikuwa kimepigwa na Kimbuga kiitwacho Namu, na miti hiyo ilikuwa imetengwa kipekee kwa ajili ya kujenga upya makao yao yaliyoharibiwa.
Ili kupata magogo hayo, akina dada wa Kutaniko la Auki walitengeneza barabara yenye upana wa meta sita, wakifyeka kichaka chenye miti mingi umbali wa karibu kilometa moja kutoka mahali pa kukatia magogo mpaka barabara kuu. Walijikakamua kwa nguvu zao zote kukata miti, wakajenga madaraja juu ya mitaro, na kuondoa vizuizi kutoka kwenye barabara hiyo
mpya. Ndipo miti iliyoteuliwa ingeweza kukatwa, kuondolewa matawi yayo, na kupasuliwa kwa mraba kwa misumeno ya minyororo.“Sisi ni Kama Chungu”
Mbao mpya zilikuwa zimekatwa sentimeta 36 mraba na meta 6.4 urefu. Lakini magogo hayo makubwa yangefikaje kwenye barabara kuu iliyokuwa umbali wa karibu kilometa moja?
Washiriki wa kutaniko waliitikia hivi: “Sisi ni kama chungu! Tukiwa na mikono ya kutosha twaweza kusafirisha chochote!” (Linganisha Mithali 6:6.) Ndugu na dada zaidi walipohitajiwa kuchukua magogo, sauti kuu ilisikika katika eneo la kukata magogo hivi: “Chungu! Chungu! Chungu!” Ndugu na dada walimiminika kutoka pande zote kuja kusaidia. Ndugu na dada arobaini wangeinua kwa mikono gogo la nusu tani na kulipeleka njiani mpaka barabara kuu, ili lichukuliwe na lori mpaka kwenye mahali pa ujenzi.
Kuweka nguzo na mihimili mahali pazo ilikuwa shughuli hatari. Kwa mara nyingine, njia ya wenyeji ya kufanya mambo ilithibitika kuwa yenye mafanikio zaidi. Baada ya kuwasilishwa kwenye mahali pa ujenzi, kila nguzo iliwekwa karibu meta tatu kutoka penye shimo refu ambamo ilipaswa kutumbukizwa ndani na kisha kuimarishwa kwa saruji.
Ndugu na dada thelathini waliinua ncha ya juu ya nguzo na kuiweka juu ya fremu yenye vipande vya mbao vilivyounganishwa pamoja. Kisha waliisukuma hiyo nguzo ardhini kwa haraka, ncha yayo ya chini ikiwa inateleza kuelekea shimo iliyokusudiwa kuingia. Ndugu wawili wajasiri sana walisimama wakishika vipande vya mbao upande wa pili wa shimo, na gogo lilipoteleza na kugonga mbao hizo, lingesimama ghafula, kwa hiyo mwendo huo ungeinua nguzo kusimama wima, na hivyo kutumbukia katika shimo la msingi.
Kosa Lageuka Kuwa Baraka
Halafu, paa iliratibiwa kuwekwa kwenye jumba. Hata hivyo, kufikia wakati huo hazina ya ujenzi ilikuwa imemalizika kabisa, na kutaniko halingeweza kununua paa ya chuma kwa ajili ya jengo hilo. Ni jambo la kushukuriwa, kwamba Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova lilipotaarifiwa kuhusu tatizo la ndugu hao, lilitoa zawadi ya dola 10,000 za U.S., zilizotosha si kununua paa tu bali pia kukamilisha Jumba la Kusanyiko.
Rehani ya dola 6,000 ililipwa kwa kampuni ya kuuza mabati kwa ajili ya paa ya chuma cha pua iliyopakwa rangi kijivu-hafifu. Ingawa paa hiyo haikuwa na rangi ya kupendeza na unene na ubora wayo haukuwa ule uliotakwa na halmashauri ya ujenzi, hiyo ndiyo tu ingeweza kununuliwa. Hata hivyo, kikundi cha ujenzi kilihuzunika, kupata vifaa vya paa ya chuma cha pua vilivyohitajiwa vilikuwa tayari vimeuzwa kwa kikundi kingine cha kidini katika Honiara kwa ajili ya ujenzi wa kanisa lao jipya. Kampuni hiyo ya ugavi iliwaomba ndugu radhi kwa mvurugo huo, lakini haikuwa na vifaa vya paa vya aina hiyo vilivyobaki akibani.
Juma moja baadaye, kampuni iliwajulisha Mashahidi kuwa akiba ya vifaa vya paa vizito na bora zaidi vilikuwa vimewasili. Lakini kwa sababu ya kosa la kampuni, kampuni ingeruhusu kutaniko kuvinunua kwa bei iliyopunguzwa sana—ambayo bajeti ya hazina ya ujenzi ingeweza kuhimili. Jambo la kutokeza hata zaidi ni kuwa, paa ya chuma cha pua ilikuwa tayari imepakwa rangi chanikiwiti yenye kupendeza, ambayo ilitakiwa na akina ndugu mwanzoni lakini hawangeweza kuinunua.
Katika Desemba 1987, Ndugu Henry Donaldson, mwenye kandarasi ya paa kutoka New Zealand aliwasili. Mradi huo ulivishwa taji zuri la paa yenye meta 1,100 za mraba. Sasa malori ya abiria yaliyokuwa yakipeleka watesaji wao yalipokuwa yakipita mahali pa ujenzi, ndugu na dada hatimaye wangeweza kuimba na kucheza dansi—wakiashiria kwa shauku jengo lao lililokuwa karibu kukamilika!
Wazia shangwe yao wakati, siku chache baadaye, jumba hilo lilipotumiwa kwa mara ya kwanza. Viv Mouritz kutoka tawi la Australia, akitumikia akiwa mwangalizi wa eneo la dunia, alipohutubia watu 593. Aliwasifu wote waliojitolea waliokuwa wamefanya kazi kwa bidii katika mradi huo mkubwa kwa roho yao ya kujidhabihu na ustahimilivu.
Kutumia Kile Kilichoko
Jumba la Kusanyiko hilo katika Malaita ni mfano wa jinsi mambo makubwa yaweza kutekelezwa bila vifaa vya kisasa vya ujenzi na vifaa vya kibiashara. Jumba hilo lasimama likiwa ithibati ya jinsi Yehova anavyobariki jitihada za wale wanaomtumaini kikamili. Katika pindi nyingi kazi iliendelea hata bila ya vifaa vya msingi zaidi, kama vile vijiko vikubwa au sepetu, ambavyo vingeonwa kuwa vya lazima kabisa katika nchi zenye utajiri zaidi.
Ilipohitajiwa kuchimba udongo wa matumbawe na kuupakia ndani ya magunia ili yasafirishwe mpaka katika mahali pa ujenzi, akina dada walichimba changarawe ya matumbawe kutoka katika shimo wakitumia vijiti vyenye ncha kali kisha wakakusanya changarawe hiyo yenye ncha kali na kuitia ndani ya magunia
kwa mikono yao mitupu. Katika siku moja tu, dada walichimba na kupakia shehena malori 13 ya tani tatu kila moja za udongo wa matumbawe!Mfano mwingine wa kutumia vile vilivyoko mkononi ni wakati gurudumu la wilibaro katika mahali pa ujenzi lilipoharibika kabisa na lingine la kubadilisha likakosekana katika Visiwa Solomoni. Hilo halikuwazuia Mashahidi hata kidogo. Baada ya kujaza wilibaro saruji, wao waliiinua juu tu na kuibeba mpaka mahali palipohitajiwa, mpaka gurudumu jingine lilipofika kutoka New Zealand majuma matano baadaye.
Hatimaye, baada ya kazi nyingi zaidi kufanywa, Jumba la Kusanyiko lilitumiwa kwa ajili ya “Haki ya Kimungu” Mkusanyiko wa Wilaya wakati wa Oktoba 1988.
Kituo chetu kifuatacho cha utalii wetu wa mahali pa ujenzi ni Honiara, kwenye kisiwa Guadalcanal.
“Katika Majuma Mawili Tu”
“Katika majuma wawili tu!” Upesi habari ilienea katika jiji la Honiara. Itikio lilikuwa lile la udadisi, mshangao, na kutia shaka. Jengo kubwa ambamo watu 1,200 waweza kutoshea laweza kujengwaje katika majuma mawili? Hilo lingewezekanaje katika kisiwa kilichoko mbali sana na vifaa vya kitekinolojia vya ulimwengu ulioendelea?
Tekinolojia ya kisasa na ustadi wa mtu mmoja-mmoja si ndivyo vilivyoleta ufanisi wa mradi huo. Hata hivyo, Jumba la Kusanyiko, lenye kinga dhidi ya kimbunga, lakini lenye kustarehesha likiwa na jukwaa na vifaa vya sauti lilihitajiwa sana katika nchi hiyo ambapo mipango ya usafiri na uhandisi unaohusu ujenzi hupangwa kwa miezi na miaka, si siku na majuma.
Msingi ulipokuwa ukijengwa, kupendezwa kwa wenyeji kulikua. Hata hivyo, wengi walitazama wakiwa na mashaka walipoanza kufahamu ukubwa wa jengo ambalo lingejengwa kwa kuangalia msingi. Waliuliza hivi: “Mtawezaje kujenga jengo hili kubwa katika majuma mawili tu?”
Upesi shehena ya vipande vikubwa vya chuma cha pua iliwasili na kupakuliwa kutoka melini. Wakuu wa serikali ya
Honiara walikuwa wenye kusaidia sana na wasikilizao sababu za wengine, wakifanya zaidi ya yale yaliyohitajiwa kwa kufafanua utaratibu wa kuingiza bidhaa kutoka ng’ambo. Pia mamlaka ya Visiwa Solomoni iliwapa kibali kikundi cha waliojitolea wapatao 60, wote wakiwa Mashahidi kutoka Australia, kuja Honiara na kufanya kazi na Mashahidi wenyeji katika kipindi cha ujenzi wenyewe cha majuma mawili. Ndugu walionyesha uthamini ulioje kwa ufikirio huo wenye fadhili na msaada wa wakuu hao!Katika Juni 7, 1991, kikundi cha ujenzi kilipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Honiara na ndugu waliokuwa na meno meupe yang’aayo yaliyokuwa kama majohari katika tabasamu za nyuso zao nyeusi, pamoja na shada la misanapichi na upendo ufanyao udugu huo wa kimataifa kuwa usio na kifani. Haya
zozote zilizokuwapo mwanzoni zilitoweka wafanyakazi wote walipoanza siku iliyofuata kujenga nyumba kubwa kwa ajili ya ibada ya Yehova. Kila fundi aliwaonyesha kwa furaha stadi zake wale waliogawiwa kufanya kazi naye. Muuzaji wa vifaa vya ujenzi alitazama jengo hilo la chuma na kusema kwa mshangao hivi: “Wakati mmoja nilikuwa na mradi wa kujenga tani 25 za chuma uliochukua miezi mitatu. Ninyi hapa mmejenga tani 30 katika siku mbili na nusu tu!”Siku 15 tu baada ya kazi kwenye Jumba la Kusanyiko lililojengwa upesi kuanza, mkutano wa kwanza ulifanywa. Ndugu na dada wageni walilazimika kuondoka upesi sana. Mandhari kwenye uwanja wa ndege ilikuwa sawa na wakati wa kuja kwao—shada la misanapichi na kila mtu alichoka kwa sababu ya kusalimiana kwa mikono na kukumbatiana, ingawa wakati huo ni wachache waliokuwa hawatokwi na machozi.
“Visiwa Vyenye Furaha” Leo
Ingawa miaka zaidi ya 35 imepita tangu habari njema ya Mungu mwenye furaha ilipofika Visiwa Solomoni, kuna visiwa vizima-vizima, kama vile Santa Isabel, Shortland, Rennell, Bellona, Tikopia, Sikaiana, na Ulawa, ambapo habari njema ya Ufalme haijahubiriwa kwa njia iliyopangwa kitengenezo. Kwa kweli, wakati umefika wa ushahidi zaidi kutolewa kwa mapana na marefu. Ingawa wenyeji wa Visiwa Solomoni wenyewe huita nchi yao “Visiwa Vyenye Furaha,” matatizo magumu yanawakabili. Kwa wenyeji wengi, hizi kwelikweli ni “nyakati za hatari [“zilizo ngumu kushughulika nazo,” NW].” (2 Tim. 3:1) Watu wamebanwa kiuchumi. Badiliko la maisha kutoka yale ya kijijini kuwa yale ya mjini limesababisha magumu ya kijamii. Watu wanatafuta majibu kwa matatizo yao, na wenye mioyo myeupe wanagundua kuwa Mashahidi wa Yehova wanaelekeza kwenye majibu sahihi, yenye kufariji kutoka chanzo cha pekee cha hekima na faraja, Neno la Mungu.
Wenyeji wengi wanaweza kuona utendaji wa roho ya Yehova miongoni mwa watu wake. Katika Auki, Malaita, walishangaa kuona kutaniko la wahubiri 60 wasio na utajiri wa vitu vya kimwili wakijenga Jumba la Kusanyiko lenye kupendeza lenye
viti 1,500 kwa msaada wa upendo wa ndugu zao wa kiroho kutoka New Zealand na Australia na msaada wa kifedha kutoka United States na Swedeni. Kama tokeo, wengi wanaopendezwa wanashirikiana na watu wa Yehova.Mara nyingi watu ambao wamesikia ngano au wameona picha za Visiwa Pasifiki Kusini huwa na dhana bandia kuvihusu. Wao huamini kuwa visiwa hivyo ni paradiso, ambapo maisha si ya jasho na ambapo kupainia ni raha mustarehe. Kwa kusikitisha, picha hizo huwa hazionyeshi mbu, usubi, vimbunga, na matetemeko ya ardhi. Huwa hazifunui unyevu ulioko wa asilimia 100, ukitokeza kuota kwa kuvu kwenye nguo, vitabu, na mali nyinginezo, wala hazitokezi wazi magonjwa ya kitropiki, nyoka, na mamba. Hivyo, hazina za Visiwa Solomoni si za kimwili. Zapatikana katika watu waliochukua msimamo kumwabudu Yehova—hivi ndivyo vile “vitu vinavyotamaniwa na mataifa”—watu wanaompenda Yehova na ambao wamerekebisha maisha zao kufanya mapenzi yake. (Hag. 2:7) Fadhili zao, nia yao ya kujifunza sheria za Mungu na kuzitumia, na ushikamanifu wao kwa Ufalme wa Mungu ndiyo mambo yafanyayo wenyeji wa Visiwa Solomoni watamanike machoni pa Yehova.
Yehova na aendelee kuibariki sana kazi ya watumishi wake wanyenyekevu, na wenye furaha kwenye “Visiwa Vyenye Furaha” vilivyoko mbali wanapofuatia furaha pekee iliyo halisi na ya kudumu, kwa kutanguliza mambo ya kiroho maishani mwao.—Mt. 5:3; 6:33.
[Maelezo ya Chini]
^ Kwa habari zaidi, ona Kitabu-Mwaka cha Mashahidi wa Yehova 1978 (Kiingereza).
[Chati katika ukurasa wa 252]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa.)
Visiwa Solomoni
1,200
1954 1
1960 135
1970 553
1980 497
1991 851
Kilele cha Wahubiri
100
1954
1960 3
1970 57
1980 69
1991 70
Wast. Mapainia
[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 208]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa.)
VISIWA SOLOMONI
KISIWA-MATUMBAWE ONTONG JAVA
Bahari ya Pasifiki Kusini
CHOISEUL
VISIWA SHORTLAND
GIZO
VISIWA NEW GEORGIA
Munda
SANTA ISABEL
MALAITA
Malu’u
Auki
GUADALCANAL
Honiara
Mkoa wa Makira
ULAWA
SAN CRISTOBAL (MAKIRA)
Mkoa wa Temotu
VISIWA REEF
VISIWA SANTA CRUZ
Lata
[Ramani]
IKWETA
PAPUA NEW GUINEA
AUSTRALIA
[Sanduku]
VISIWA SOLOMONI
Jiji Kuu: Honiara, Guadalcanal
Lugha Rasmi: Pidgini ya Visiwa Solomoni na Kiingereza
Dini Kubwa: Anglikana
Idadi: 328,723
Ofisi ya Tawi: Honiara
[Picha katika ukurasa wa 210]
Bandari ya Honiara kwenye pwani ya kaskazini ya Guadalcanal
Watoto wa Visiwa Solomoni
[Picha katika ukurasa wa 212]
Ofisi ya Tawi katika Honiara katika kisiwa Guadalcanal
[Picha katika ukurasa wa 213]
Joan na Bob Seccombe wakiwa mbele ya ofisi ya tawi ya kwanza
[Picha katika ukurasa wa 217]
Habari njema zimehubiriwa kwa bidii katika visiwa sita kati ya vile vikuu na katika visiwa vingi vidogo
[Picha katika ukurasa wa 218]
Jumba la Ufalme katika Gizo, Mkoa wa Magharibi. Miti ya vichakani na majani yaliyofumwa au kusokotwa ya mvumo hutumiwa kujenga baadhi ya majumba
[Picha katika ukurasa wa 227]
Majani ya taro hutumiwa kama miavuli. Ujumbe waweza pia kuandikwa katika majani hayo
[Picha katika ukurasa wa 233]
Elson Site, painia wa pekee, na familia yake
[Picha katika ukurasa wa 243]
Magogo yakibebwa kutoka misitu yenye matope-matope na kukatwa mraba kwa misumeno ya minyororo yapakiwa katika lori. Gogo lililokatwa kwa mraba (nguzo ya ukuta) linatiwa katika shimo la msingi katika Jumba la Kusanyiko la Auki
[Picha katika ukurasa wa 244]
Mikingiko mikubwa ya paa yenye uzito wa kufikia tani tano hutengenezwa kwa kuunganisha magogo manane pamoja. Mikingiko hiyo huwekwa juu ya nguzo yenye urefu wa meta 6 bila msaada wa vifaa vizito vya ujenzi
[Picha katika ukurasa wa 245]
Jumba la Kusanyiko lililokamilika lenye viti 1,500 katika Auki, Malaita
[Picha katika ukurasa wa 249]
Fremu inayoweza kustahimili vimbunga na matetemeko ya ardhi inaendelea kujengwa
“Jengo Kubwa” latoshea 1,200 katika Honiara, Guadalcanal
[Picha katika ukurasa wa 251]
Halmashauri ya Tawi. Kutoka kushoto kuelekea kulia, James Ronomaelana, Josef Neuhardt, na Rodney Fraser