SURA YA 14
Kwa Nini Tuwe Wenye Kusamehe
JE, MTU yeyote amewahi kukukosea?— Je, alikuumiza au kukuambia jambo lisilo la fadhili?— Je, unapaswa kumtendea kwa njia isiyo ya fadhili kama alivyokutendea?—
Watu wengi wanapoumizwa na mtu, wao pia wanalipiza kwa kumwumiza yule mtu. Lakini Yesu alitufundisha tuwasamehe wale wanaotukosea. (Mathayo 6:12) Vipi ikiwa mtu anatukosea mara nyingi? Tumsamehe mara ngapi?—
Hilo ndilo Petro alitaka kujua. Kwa hiyo siku moja alimwuliza Yesu: ‘Je, nimsamehe mpaka mara saba?’ Mara saba haitoshi. Yesu akasema: ‘Unapaswa kumsamehe mpaka mara 77’ iwapo mtu anakukosea mara nyingi hivyo.
Hiyo ni mara nyingi sana! Hatuwezi hata kuhesabu makosa mengi hivyo ambayo mtu alitufanyia, sivyo? Na hilo ndilo somo ambalo Yesu alitaka tujifunze: Hatupaswi kujaribu kuhesabu makosa ambayo huenda wengine wakatufanyia. Wakiomba msamaha, tuwasamehe.
Yesu alitaka kuwaonyesha wanafunzi wake jinsi ilivyo muhimu kusamehe. Kwa hiyo baada ya kujibu swali la
Petro, aliwasimulia wanafunzi wake hadithi moja.Hapo zamani kulikuwa na mfalme mzuri mwenye huruma sana. Hata alikuwa akiwakopesha watumwa wake pesa walipokuwa na uhitaji. Lakini siku moja mfalme akataka watumwa wake waliokuwa na madeni yake wamlipe. Basi mtumwa mmoja aliyekuwa na deni la vipande milioni 60 vya fedha za mfalme aliletwa ndani. Hizo ni pesa nyingi wee!
Lakini mtumwa huyo alikuwa ametumia pesa zote na kwa hiyo hangeweza kumlipa mfalme pesa zake. Basi mfalme akatoa amri mtumwa huyo auzwe. Mfalme akasema pia kwamba mke wa mtumwa huyo na watoto wake wauzwe pamoja na mali zake zote. Kisha, mfalme angepewa pesa ambazo zingepatikana. Unafikiri mtumwa huyo alihisije?—
Alimpigia mfalme magoti na kumwomba: ‘Tafadhali, uwe na subira nami nitakulipa kila kitu.’ Kama ungalikuwa mfalme huyo, ungalimtendeaje mtumwa huyo?— Mfalme alimhurumia. Kwa hiyo mfalme akamsamehe. Akamwambia mtumwa huyo asilipe pesa zozote, hata kimoja cha vipande hivyo milioni 60 vya fedha. Bila shaka mtumwa huyo alifurahi sana kusikia hivyo.
Lakini mtumwa huyo alifanyaje? Alitoka na kukutana na mtumwa mwingine ambaye alikuwa na deni lake la vipande 100 tu vya fedha. Akamshika shingo na kuanza kumnyonga, akisema: ‘Nilipe pesa zangu ulizo nazo!’ Unaweza kuwazia mtu anayefanya jambo kama hilo, hasa baada ya kusamehewa deni kubwa na mfalme?—
Yule mtumwa aliyekuwa na deni la vipande 100 vya fedha za mwenzake alikuwa maskini. Hangeweza kulipa pesa hizo mara moja. Basi akaanguka miguuni pa mtumwa mwenzake na kumwomba: ‘Tafadhali, uwe na subira nami nitakulipa.’ Je, mtu huyo alimpa mtumwa mwenzake wakati zaidi?— Wewe ungefanyaje?—
Mtu huyo hakuwa na huruma kama yule mfalme. Alitaka pesa zake mara moja. Na kwa sababu mtumwa mwenzake hangeweza kulipa, aliamuru afungwe gerezani. Watumwa wengine waliona mambo hayo yote
yakitendeka na hawakufurahi. Walimhurumia mtumwa yule aliyekuwa gerezani. Basi wakaenda na kumwambia mfalme mambo hayo.Mfalme pia hakufurahia jambo hilo. Mtumwa huyo asiyesamehe alimuudhi sana. Basi akamwita akamwambia: ‘Ewe mtumwa mwovu, je, sikukusamehe deni lote ulilo nalo? Je, hukupaswa kumsamehe mtumwa mwenzako?’
Mtumwa huyo asiyesamehe angalijifunza somo kutoka kwa yule mfalme mzuri. Lakini hakufanya hivyo. Basi sasa mfalme akaamuru afungwe gerezani hadi wakati ambapo angelipa vile vipande milioni 60 vya fedha. Na bila shaka, akiwa gerezani hawezi kamwe kupata pesa za kumlipa mfalme. Kwa hiyo angekaa huko mpaka afe.
Yesu alipomaliza kusema hadithi hiyo, aliwaambia wanafunzi wake: ‘Baba yangu wa mbinguni atashughulika nanyi pia kwa njia hiyo ikiwa kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.’ —Mathayo 18:21-35.
Unapaswa kujua kwamba sote tuna deni kubwa mbele za Mungu. Kwa kweli, Mungu ndiye ametupatia uhai! Basi tunapolinganisha deni letu kwa Mungu, watu wengine wana madeni madogo kwetu. Deni letu walilo nalo ni kama vipande 100 vya fedha ambavyo mtumwa yule alipaswa kumlipa mwenzake. Lakini deni letu kwa Mungu kwa sababu ya makosa ambayo sisi hufanya ni kama vile vipande milioni 60 vya fedha ambavyo yule mtumwa alipaswa kumlipa mfalme.
Mungu ana fadhili sana. Ijapokuwa tumefanya makosa, yeye hutusamehe. Halipizi kwa kutuua milele. Lakini tunapaswa kukumbuka somo hili: Mungu hutusamehe tu ikiwa tunawasamehe wanaotukosea. Hilo ni jambo tunalopaswa kufikiria, sivyo?—
Basi ikiwa mtu anakukosea lakini anakuomba msamaha, utafanya nini? Je, utamsamehe?— Vipi akikukosea mara nyingi? Bado utaendelea kumsamehe?—
Iwapo ni sisi tunaomba mtu msamaha, tungependa atusamehe, sivyo?— Basi na sisi tunapaswa kumsamehe pia. Hatupaswi kusema tu kwamba tumemsamehe, bali tunapaswa kumsamehe kikweli kutoka moyoni. Tunapowasamehe wengine, tunaonyesha kwamba tunataka kweli kuwa wafuasi wa Mwalimu Mkuu.
Ili kuelewa umuhimu wa kuwa mwenye kusamehe tusome pia Mithali 19:11; Mathayo 6:14, 15; na Luka 17:3, 4.