SEHEMU YA 4
Mungu Afanya Agano na Abrahamu
Abrahamu aonyesha imani kwa kumtii Mungu; Yehova aahidi kumbariki na kuzidisha uzao wake
MIAKA 350 baada ya Gharika ya siku za Noa, Abrahamu alikuwa akiishi katika jiji lenye ufanisi la Uru, eneo ambalo leo linaitwa Iraki. Abrahamu alikuwa mtu mwenye imani ya pekee. Hata hivyo imani yake ilijaribiwa.
Yehova alimwambia Abrahamu aondoke katika nchi alimozaliwa na kwenda nchi asiyoijua, nchi ya Kanaani. Abrahamu alitii bila kusita. Alikusanya watu wa nyumba yake, kutia ndani mke wake, Sara, na mpwa wake Loti, akafunga safari ndefu na kwenda kuishi katika mahema huko Kanaani. Katika agano alilofanya pamoja na Abrahamu, Yehova alimwahidi kwamba atamfanya kuwa taifa kubwa, na kwamba familia zote za dunia zitajibariki kupitia kwake, nao uzao wake utaimiliki nchi ya Kanaani.
Abrahamu na Loti walipata ufanisi, wakajikusanyia kondoo na ng’ombe wengi. Abrahamu alimtanguliza Loti kwa kumpa nafasi achague eneo analotaka. Loti alichagua mkoa wenye rutuba wa Mto Yordani na kwenda kukaa karibu na jiji la Sodoma. Lakini, watu wa Sodoma walikuwa wapotovu kiadili—watenda-dhambi nzito mbele za Yehova.
Yehova Mungu alimhakikishia Abrahamu baadaye kwamba uzao wake ungeongezeka na kuwa kama nyota za mbinguni. Abrahamu aliamini ahadi hiyo. Hata hivyo, Sara, mke wake mpendwa hakuwa na mtoto. Kisha, Abrahamu alipokuwa na umri wa miaka 99, naye Sara akikaribia umri wa miaka 90, Mungu alimwambia Abrahamu kwamba Sara atapata mtoto. Maneno ya Mungu yalitimia. Sara akamzaa Isaka. Abrahamu alikuwa na watoto wengine, hata hivyo, yule Mkombozi aliyeahidiwa katika Edeni angetokana na ukoo wa Isaka.
Wakati huohuo, Loti na familia yake walikuwa wakiishi Sodoma, lakini Loti hakuwa kama wakaaji wa jiji hilo waliokuwa na maadili mapotovu. Yehova alipoamua kutekeleza hukumu juu ya Sodoma, aliwatuma malaika wawili wakamwonye Loti kuhusu uharibifu uliokuwa ukikaribia. Malaika hao walimhimiza Loti na familia yake wakimbie kutoka Sodoma na wasitazame nyuma. Kisha Mungu akanyesha mvua ya moto na kiberiti juu ya Sodoma na jiji jirani la Gomora lililojaa uovu. Wakaaji wote wa majiji hayo wakaangamia. Loti na binti zake wawili waliokoka. Mke wa Loti alitazama nyuma, huenda akitamani vitu alivyokuwa ameviacha. Kutotii huko kulimfanya apoteze uhai wake.
—Inatoka kwenye Mwanzo 11:10–19:38.