SURA YA 61
Yesu Amponya Mvulana Mwenye Roho Mwovu
MATHAYO 17:14-20 MARKO 9:14-29 LUKA 9:37-43
-
IMANI YENYE NGUVU ILIHITAJIKA ILI KUMPONYA MVULANA MWENYE ROHO MWOVU
Yesu, Petro, Yakobo na Yohana wanaposhuka kutoka mlimani, wanakutana na umati mkubwa. Kuna tatizo. Waandishi wamewazunguka wanafunzi wakibishana nao. Watu wanashangaa kumwona Yesu, nao wanakimbia kwenda kumsalimu. Yesu anawauliza: “Mnabishania nini?”—Marko 9:16.
Mwanamume fulani katika umati huo anapiga magoti mbele ya Yesu na kusema: “Mwalimu, nilimleta mwanangu kwako kwa sababu ana roho anayemfanya awe bubu. Kila mara anapomshambulia humwangusha chini, naye hutoa povu mdomoni na kusaga meno yake na kuishiwa nguvu. Niliwaambia wanafunzi wako wamfukuze, lakini hawakuweza.”—Marko 9:17, 18.
Inaonekana waandishi wanawashutumu wanafunzi kwa sababu wameshindwa kumponya mvulana huyo, labda hata wanawadhihaki. Basi badala ya kumjibu baba huyo aliye na wasiwasi, Yesu anauambia umati: “Enyi kizazi kisicho na imani na kilichopotoka, nitaendelea kuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini?” Maneno hayo mazito yanawahusu waandishi ambao walikuwa wakiwasumbua wanafunzi wake kabla hajafika. Akimgeukia yule baba aliyehuzunika, Yesu anasema: “Mleteni hapa.”—Mathayo 17:17.
Mvulana huyo anapomkaribia Yesu, roho mwovu aliyekuwa akimsumbua anamwangusha chini na kumfanya agaegae. Yule mvulana anaendelea kujiviringisha chini, akitoa povu mdomoni. “Jambo hili limekuwa likitokea kwa muda gani?” Yesu anamwuliza yule baba. Anajibu: “Tangu utotoni, naye humwangusha ndani ya moto na ndani ya maji ili amuue.” Mwanamume huyo anamsihi hivi: “Ikiwa unaweza kufanya chochote, tuhurumie na utusaidie.”—Marko 9:21, 22.
Baba huyo amekata tamaa kwa sababu hata wanafunzi wa Yesu wameshindwa kumsaidia. Akijibu ombi la mwanamume huyo aliyekata tamaa, Yesu anamtia moyo kwa kumhakishia hivi: “Maneno hayo, ‘Ikiwa unaweza’? Mambo yote yanawezekana kwa mtu mwenye imani.” Mara moja baba huyo anapaza sauti: “Nina imani! Nisaidie mahali ambapo ninahitaji imani!”—Yesu anagundua kwamba umati unamkimbilia. Watu hao wote wakiwa wanatazama, Yesu anamkemea yule roho mwovu: “Wewe roho bubu na kiziwi, ninakuagiza umtoke mtoto huyu na usimwingie tena!” Anapotoka, yule roho mwovu anamfanya mvulana huyo apige mayowe na kugaagaa sana. Kisha yule mvulana analala hapo bila kutikisika. Wanapoona hivyo, watu wengi wanasema: “Amekufa!” (Marko 9:25, 26) Lakini Yesu anapomshika mkono mvulana huyo, anaamka na ‘anapona kuanzia saa hiyo.’ (Mathayo 17:18) Ni wazi kwamba watu wanashangazwa na mambo ambayo Yesu anafanya.
Hapo awali, Yesu alipowatuma wanafunzi wake wakahubiri, walikuwa na uwezo wa kufukuza roho waovu. Sasa wakiwa ndani ya nyumba faraghani, wanamuuliza: “Kwa nini tulishindwa kumfukuza?” Yesu anaeleza kwamba ni kwa sababu walikosa imani, anawaambia: “Roho wa aina hii hawezi kutoka isipokuwa kwa sala.” (Marko 9:28, 29) Walihitaji kuwa na imani yenye nguvu na kusali ili Mungu awape nguvu zilizohitajika kumfukuza yule roho mwovu mwenye nguvu.
Yesu anamalizia hivi: “Kwa kweli ninawaambia, mkiwa na imani inayolingana na mbegu ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka, na hakuna jambo litakalowashinda.” (Mathayo 17:20) Imani ina nguvu kwelikweli!
Vikwazo na hali ngumu zinazozuia maendeleo katika utumishi wa Yehova zinaweza kuonekana kuwa kubwa sana na zisizoweza kuondolewa kama mlima halisi. Hata hivyo, tukisitawisha imani, tunaweza kushinda vikwazo na hali hizo ngumu zilizo kama mlima.