SURA YA 21
Katika Sinagogi Huko Nazareti
-
YESU ASOMA KITABU CHA KUKUNJWA CHA ISAYA
-
WATU WA NAZARETI WAJARIBU KUMUUA YESU
Bila shaka watu wamesisimka huko Nazareti. Kabla hajaondoka kwenda kubatizwa na Yohana karibu mwaka mmoja uliopita, Yesu alikuwa seremala katika eneo hili. Lakini sasa anajulikana kama mtu anayefanya kazi zenye nguvu. Wakaaji wa huko wanatamani kumwona akifanya baadhi ya kazi hizo miongoni mwao.
Matarajio yao yanaongezeka wakati Yesu, kama desturi yake, anaenda katika sinagogi la huko. Ibada inatia ndani kusali na kusoma vitabu vya Musa, kama inavyofanywa “katika masinagogi kila sabato.” (Matendo 15:21) Pia, visehemu vya vitabu vya manabii husomwa. Yesu anaposimama ili kusoma, huenda anawatambua watu wengi kwa sababu alihudhuria sinagogi hili kwa miaka mingi. Anapewa kitabu cha kukunjwa cha nabii Isaya. Anapata sehemu inayosema kuhusu Yule aliyetiwa mafuta na roho ya Yehova, simulizi ambalo leo linapatikana kwenye Isaya 61:1, 2.
Yesu anasoma kuhusu Yule aliyeahidiwa ambaye angewatangazia mateka kuachiliwa, vipofu kuweza kuona, na kutangaza kuja kwa mwaka wa Yehova unaokubalika. Yesu anamkabidhi mtumishi kile kitabu cha kukunjwa kisha anaketi chini. Watu wote wanamtazama kwa makini. Anazungumza, labda kwa muda fulani, na maelezo yake yanatia ndani maneno haya muhimu: “Leo andiko hili ambalo mmetoka kusikia limetimia.”—Luka 4:21.
Watu wanashangazwa na “maneno yenye neema [yanayotoka] kinywani mwake,” nao wanaambiana: “Huyu ni mwana wa Yosefu, sivyo?” Lakini akitambua kwamba wanataka kuona akifanya miujiza kama ile waliyosikia, Yesu anaendelea kusema: “Bila shaka mtautumia mfano huu kwangu, ‘Daktari, jiponye mwenyewe. Fanya pia katika eneo la nyumbani kwenu mambo tuliyosikia yamefanywa huko Kapernaumu.’” (Luka 4:22, 23) Inaelekea majirani wa zamani wa Yesu wanaona kwamba uponyaji unapaswa kuanzia nyumbani, ili kuwanufaisha watu wake kwanza. Basi huenda wanafikiri Yesu amewapuuza.
Akitambua jambo wanalofikiria, Yesu anataja baadhi ya matukio katika historia ya Israeli. Kulikuwa na wajane wengi huko Israeli katika siku za Eliya, anasema, lakini Eliya hakutumwa kwa yeyote kati yao. Badala yake, alienda kwa mjane asiye Mwisraeli huko Sarefathi, mji ulio karibu na Sidoni, ambako Eliya alifanya muujiza uliookoa uhai. (1 Wafalme 17:8-16) Na katika siku za Elisha, kulikuwa na watu wengi wenye ukoma huko Israeli, lakini nabii huyo alimponya Naamani Msiria peke yake.—2 Wafalme 5:1, 8-14.
Watu hao kutoka mji wa nyumbani wa Yesu watatendaje kutokana na kile wanachoona kuwa ulinganifu usiofaa wa kihistoria unaofunua ubinafsi na ukosefu wao wa imani? Watu walio katika sinagogi wanakasirika, wanasimama, na kumtoa Yesu nje ya jiji haraka. Wanampeleka kwenye ukingo wa mlima ambao jiji la Nazereti limejengwa, nao wanajaribu kumtupa chini. Lakini Yesu anaponyoka kutoka katikati yao na kuondoka akiwa salama. Sasa Yesu anateremka kwenda Kapernaumu, kwenye ufuo wa kaskazini magharibi wa Bahari ya Galilaya.