SURA YA 125
Yesu Apelekwa kwa Anasi, Kisha kwa Kayafa
MATHAYO 26:57-68 MARKO 14:53-65 LUKA 22:54, 63-65 YOHANA 18:13, 14, 19-24
-
YESU APELEKWA KWA KUHANI MKUU WA ZAMANI ANASI
-
SANHEDRINI YAFANYA KESI ISIYO HALALI
Baada ya Yesu kufungwa kama mhalifu, anapelekwa kwa Anasi, ambaye alikuwa kuhani mkuu wakati mvulana Yesu alipowashangaza walimu hekaluni. (Luka 2:42, 47) Baadaye, baadhi ya wana wa Anasi walitumikia wakiwa wakuu wa makuhani, lakini sasa mkwe wake, Kayafa, ndiye aliye na cheo hicho.
Yesu akiwa nyumbani kwa Anasi, Kayafa anapata muda wa kuwakusanya washiriki wa Sanhedrini. Mahakama hiyo yenye washiriki 71 inatia ndani kuhani mkuu na wengine waliowahi kuwa na cheo hicho.
Anasi anamhoji Yesu “kuhusu wanafunzi wake na kuhusu mafundisho yake.” Yesu anamjibu hivi: “Nimezungumza na ulimwengu hadharani. Sikuzote nilifundisha katika sinagogi na hekaluni, ambapo Wayahudi wote hukusanyika, nami sikusema jambo lolote kwa siri. Kwa nini unaniuliza? Waulize wale waliosikia nilichowaambia.”—Yohana 18:19-21.
Ofisa aliyesimama hapo karibu anampiga Yesu kofi usoni na kumkemea hivi: “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu mkuu wa makuhani?” Lakini Yesu akijua kwamba hajafanya kosa, anajibu hivi: “Ikiwa nimesema vibaya, toa ushahidi kuhusu kosa hilo; lakini ikiwa nimesema jambo lililo sawa, kwa nini unanipiga?” (Yohana 18:22, 23) Kisha Anasi anaagiza Yesu apelekwe kwa mkwe wake, Kayafa.
Kufikia sasa washiriki wote wa Sanhedrini—kuhani mkuu wa sasa, wazee wa watu, na waandishi—wamekusanyika. Wamekutana nyumbani kwa Kayafa. Si halali kufanya kesi kama hiyo usiku wa Pasaka, lakini jambo hilo haliwazuii kutimiza kusudi lao baya.
Hiki ni kikundi kisichofuata haki. Baada ya Yesu kumfufua Lazaro, Sanhedrini iliamua kwamba Yesu anapaswa kuuawa. (Yohana 11:47-53) Na siku chache zilizopita, viongozi wa kidini walipanga njama ya kumkamata Yesu na kumuua. (Mathayo 26:3, 4) Naam, hata kabla kesi yake haijaanza, tayari Yesu amehukumiwa kifo!
Zaidi ya kufanya mkutano usio halali, kuhani mkuu na washiriki wengine wa Sanhedrini wanatafuta mashahidi watakaotoa ushahidi wa uwongo katika kesi ya Yesu. Wanawapata wengi, lakini ushahidi wao unatofautiana. Mwishowe, wawili wanajitokeza na kusema: “Tulimsikia akisema, ‘Nitaliangusha chini hekalu hili lililojengwa kwa mikono, na kwa siku tatu nitajenga lingine ambalo halijajengwa kwa mikono.’” (Marko 14:58) Hata hivyo, bado watu hao hawakubaliani kabisa.
Kayafa anamuuliza hivi Yesu: “Kwa nini hujibu? Watu hawa wanashuhudia nini kukuhusu?” (Marko 14:60) Yesu anakaa kimya anapokabili mashtaka hayo ya uwongo kutoka kwa mashahidi ambao mashtaka yao yanatofautiana. Basi Kuhani Mkuu Kayafa anatumia mbinu nyingine.
Kayafa anajua kwamba Wayahudi hawakubaliani na mtu yeyote anayedai kuwa Mwana wa Mungu. Hapo awali, Yesu alipomwita Mungu Baba yake, Wayahudi walitaka kumuua kwa sababu walidai kwamba alikuwa “akijifanya kuwa sawa na Mungu.” (Yohana 5:17, 18; 10:31-39) Kayafa anajua jambo hilo, basi kwa ujanja anamwamuru Yesu hivi: “Ninakuapisha mbele za Mungu aliye hai utuambie kama wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu!” (Mathayo 26:63) Bila shaka, Yesu alisema kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. (Yohana 3:18; 5:25; 11:4) Asipofanya hivyo sasa, hilo linaweza kuonyesha kwamba anakana kuwa yeye ni Mwana wa Mungu na kwamba ndiye Kristo. Basi Yesu anasema: “Mimi ndiye; nanyi mtamwona Mwana wa binadamu akiwa ameketi kwenye mkono wa kuume wa nguvu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni.”—Marko 14:62.
Papo hapo, Kayafa anayararua mavazi yake na kusema: “Amekufuru! Tunahitaji mashahidi wengine wa nini? Tazama! Sasa mmemsikia akikufuru. Mnaonaje?” Sanhedrini inatoa hukumu hii isiyo ya haki: “Anastahili kufa.”—Mathayo 26:65, 66.
Kisha wanaanza kumdhihaki Yesu na kumpiga ngumi. Wengine wanampiga makofi usoni na kumtemea mate usoni. Baada ya kuufunika uso wake na kumpiga makofi, wanamdhihaki hivi: “Toa unabii! Ni nani aliyekupiga?” (Luka 22:64) Huyu ni Mwana wa Mungu anayetendewa vibaya katika kesi isiyo halali inayofanywa usiku!