SURA YA 118
Wabishana Kuhusu Aliye Mkuu Zaidi
MATHAYO 26:31-35 MARKO 14:27-31 LUKA 22:24-38 YOHANA 13:31-38
-
YESU ATOA USHAURI KUHUSU CHEO
-
YESU ATABIRI KWAMBA PETRO ATAMKANA
-
UPENDO UNAWATAMBULISHA WAFUASI WA YESU
Katika jioni yake ya mwisho pamoja na mitume wake, Yesu amewafundisha somo muhimu kuhusu unyenyekevu kwa kuwaosha miguu. Kwa nini jambo hilo linafaa? Ni kwa sababu wana udhaifu fulani. Wanampenda Mungu, lakini bado wanahangaika kuhusu aliye mkuu zaidi kati yao. (Marko 9:33, 34; 10:35-37) Udhaifu huo unaonekana tena jioni hii.
Mitume wanakuwa na “bishano kali kuhusu ni nani aliye mkuu zaidi kati yao.” (Luka 22:24) Bila shaka, Yesu anahuzunika sana anapoona wakibishana tena! Anafanya nini?
Badala ya kuwakemea mitume kwa sababu ya mtazamo na tabia yao, Yesu anajadiliana nao kwa subira: “Wafalme wa mataifa hupiga ubwana juu yao, na wale walio na mamlaka juu yao huitwa Wafadhili. Hata hivyo, ninyi hampaswi kuwa hivyo. . . . Kwa maana ni nani aliye mkuu zaidi, yule anayekula au yule anayehudumu?” Kisha Yesu anawakumbusha mfano ambao amewawekea sikuzote, anasema: “Lakini mimi ni kama mtu anayehudumu kati yenu.”—Luka 22:25-27.
Ingawa hawajakamilika, mitume wameshikamana na Yesu katika hali nyingi ngumu. Kwa hiyo, anasema: “Ninafanya agano pamoja nanyi, kama Baba yangu alivyofanya agano pamoja nami, kwa ajili ya ufalme.” (Luka 22:29) Wanaume hao ni wafuasi washikamanifu wa Yesu. Anawahakikishia kwamba kupitia agano analofanya kati yake nao, watatawala pamoja naye katika Ufalme.
Ingawa mitume wana tazamio hilo zuri, wao bado ni wanadamu na hawajakamilika. Yesu anawaambia: “Shetani anataka kuwapata ninyi nyote ili awapepete kama ngano,” ambayo hutawanyika inapopepetwa. (Luka 22:31) Pia anawaonya hivi: “Ninyi nyote mtakwazika kuhusiana nami usiku wa leo, kwa maana imeandikwa: ‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo wa kundi watatawanyika.’”—Mathayo 26:31; Zekaria 13:7.
Petro akiwa na uhakika anakataa akisema: “Hata wengine wote wakikwazika kuhusiana nawe, mimi sitakwazika kamwe!” (Mathayo 26:33) Yesu anamwambia Petro kwamba kabla jogoo hajawika mara mbili usiku huo, Petro atamkana. Hata hivyo, Yesu anasema: “Nimeomba dua kwa ajili yako ili imani yako isidhoofike; nawe utakaporudi, watie nguvu ndugu zako.” (Luka 22:32) Lakini Petro anasema tena kwa ujasiri: “Hata nikilazimika kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” (Mathayo 26:35) Wale mitume wengine wanasema vivyo hivyo.
Yesu anawaambia hivi wanafunzi wake: “Nipo pamoja nanyi muda kidogo zaidi. Mtanitafuta; na kama nilivyowaambia Wayahudi, ninawaambia ninyi pia, ‘Ninakoenda hamwezi kuja.’” Kisha anasema: “Ninawapa ninyi amri mpya, kwamba mpendane; kama vile ambavyo nimewapenda, nanyi mpendane vivyo hivyo. Kwa jambo hili wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu—mkiwa na upendo miongoni mwenu.”—Yohana 13:33-35.
Petro anapomsikia Yesu akisema kwamba atakuwa pamoja nao muda kidogo tu, anamuuliza: “Bwana, unaenda wapi?” Yesu anajibu: “Ninakoenda huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.” Petro anashangaa kisha anasema: “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Nitatoa uhai wangu kwa ajili yako.”—Yohana 13:36, 37.
Sasa Yesu anazungumzia wakati ambapo aliwatuma mitume katika kampeni ya kuhubiri huko Galilaya bila mfuko wa pesa au mfuko wa chakula. (Mathayo 10:5, 9, 10) Anawauliza: “Je, mlikosa chochote?” Wanajibu: “Hapana!” Lakini watafanya nini katika siku zijazo? Yesu anawaagiza: “Yule aliye na mkoba wa pesa au mfuko wa chakula aubebe, na yule asiye na upanga, auze vazi lake la nje anunue upanga. Kwa maana ninawaambia mambo yaliyoandikwa kunihusu yatatimia, yaani, ‘Naye alihesabiwa pamoja na waasi sheria.’ Kwa maana hilo linatimia kunihusu.”—Luka 22:35-37.
Yesu anazungumzia wakati ambapo atatundikwa kwenye mti pamoja na watenda maovu, au waasi sheria. Baada ya hapo, wafuasi wake watateswa sana. Wanafikiri kwamba wako tayari nao wanasema: “Bwana, tazama! hapa pana panga mbili.” Anawaambia: “Inatosha.” (Luka 22:38) Panga mbili walizo nazo zitampa Yesu fursa ya kuwafundisha jambo lingine muhimu.