SURA YA 10
Familia ya Yesu Yasafiri Kwenda Yerusalemu
-
YESU AKIWA NA UMRI WA MIAKA KUMI NA MIWILI AWAHOJI WALIMU
-
YESU ANAMWITA YEHOVA “BABA YANGU”
Ni majira ya kuchipua. Hivyo, ni wakati wa familia ya Yosefu, pamoja na marafiki na watu wa ukoo kufunga safari yao ya kila mwaka kwenda Yerusalemu. Wanaenda huko kusherehekea Pasaka, kama Sheria ilivyoagiza. (Kumbukumbu la Torati 16:16) Kutoka Nazareti kushuka mpaka Yerusalemu ni safari ya kilomita 120 hivi. Ni wakati wenye shughuli nyingi na wenye kusisimua kwa kila mmoja. Yesu ana umri wa miaka 12 sasa, na anatazamia kwa hamu sana sherehe hiyo na fursa ya kuwa karibu tena na hekalu.
Kwa Yesu na familia yake, Pasaka sio tukio la siku moja tu. Siku inayofuata Pasaka ni mwanzo wa siku saba za Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu. (Marko 14:1) Kipindi hicho kinaonwa kuwa sehemu ya majira ya Pasaka. Wanatumia majuma mawili hivi kusafiri kutoka nyumbani kwao Nazareti, kukaa Yerusalemu na kurudi tena nyumbani. Lakini mwaka huu, wanatumia muda mrefu zaidi kwa sababu ya tukio linalomhusu Yesu. Jambo hilo linatokea wakati wa safari ya kurudi kutoka Yerusalemu.
Wakiwa safarini, Yosefu na Maria wanafikiri kwamba Yesu yuko pamoja na kikundi cha watu wa ukoo na marafiki wanaosafiri pamoja kuelekea kaskazini. Hata hivyo, wanaposimama usiku ili kupumzika, hawamwoni Yesu. Basi wanaanza kumtafuta miongoni mwa wasafiri wenzao, lakini haonekani. Mvulana wao hayupo! Yosefu na Maria wanarudi tena Yerusalemu kumtafuta.
Wanamtafuta kwa siku nzima bila kumpata. Vilevile hawampati siku ya pili. Mwishowe, siku ya tatu wanamwona mwana wao katika hekalu, ambalo lina vyumba vingi. Wanamwona Yesu akiwa ameketi katikati ya baadhi ya walimu wa Kiyahudi. Anasikiliza, akiuliza maswali, na kuwashangaza kwa uelewaji wake.
“Mwanangu, kwa nini umetutendea hivi?” Maria anauliza. “Mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta tukiwa na wasiwasi mwingi.”—Luka 2:48.
Yesu anashangaa kwamba hawakujua mahali ambapo angekuwa. Anauliza: “Kwa nini mlikuwa mkinitafuta? Je, hamkujua kwamba ninapaswa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?”—Luka 2:49.
Kwa kuwa sasa wamempata, Yesu anarudi nyumbani Nazareti akiwa na Yosefu na Maria naye anaendelea kujitiisha kwao. Anazidi kuwa na hekima na kukua kimwili. Ingawa bado ana umri mdogo, ana kibali cha Mungu na wanadamu. Naam, tangu akiwa mtoto na kuendelea, Yesu aliweka mfano mzuri si kwa kupenda tu mambo ya kiroho bali pia kwa kuwaheshimu wazazi wake.