KUUTAZAMA ULIMWENGU
Marekani
Kulingana na ripoti ya Wizara ya Ulinzi wa Ndani na Usalama ya Marekani, katika muda wa miaka kumi iliyopita, wafanyakazi wa kulinda usalama katika viwanja vya ndege walizuia vitu milioni 50 vilivyopigwa marufuku visiingizwe nchini. Katika mwaka wa 2011 peke yake, wafanyakazi hao walizuia bunduki zaidi ya 1,200 zisiingizwe kwenye ndege. Wamiliki wengi wa silaha hizo walisema kwamba walikuwa wamesahau wamebeba bunduki.
Brazili
Wasimamizi wa shule wameanza kuweka vifaa vidogo sana vya kielektroniki katika sare za watoto wa shule ili kuwazuia wasikose kwenda shuleni bila ruhusa. Mzazi hupokea ujumbe mfupi unaotumwa na sensa iliyo kwenye lango la shule mtoto anapowasili shuleni, naye hupokea ujumbe tofauti ikiwa mtoto amechelewa kufika shuleni kwa dakika 20.
Norway
Kanisa la Kilutheri limeachishwa kuwa dini rasmi ya serikali nchini Norway. Kwa mara ya kwanza, Bunge la Norway lilipiga kura ili kurekebisha katiba na kupunguza uhusiano wa karibu uliopo kati ya Kanisa na Serikali.
Jamhuri ya Cheki
Katika uchunguzi mmoja uliofanywa katika Jamhuri ya Cheki asilimia 66 ya wafanyakazi walisema wanahisi kwamba lazima wajibu simu, barua-pepe, au ujumbe wa simu unaohusiana na kazi wakati hawako kazini. Asilimia 33 wanasema kwamba wanahisi ni ukaidi kutojibu mara moja.
India
Licha ya ongezeko la karibu asilimia 50 la uzalishaji wa chakula katika miaka 20 iliyopita na akiba kubwa ya tani milioni 71 za mchele na ngano, bado India inapata shida kuwalisha raia zake. Ni asilimia 40 hivi tu ya akiba ya nafaka huwafikia watu. Ufisadi na uharibifu wa chakula ni baadhi ya mambo yanayochangia tatizo hilo.